Binti Nuru Omari aliyeibuliwa.
BINTI
aitwaye Nuru Omari anayedaiwa kufariki dunia mwaka 2010 ameibuliwa hivi
karibuni wilayani Mkuranga, Mkoa wa Pwani na mganga akiwa hai kwenye
banda kuukuu.
Tukio hilo limetokea kwenye Kijiji cha Kalole, Tarafa ya Kisiju, walayani humo.
Kwa mujibu wa baba wa binti huyo, Omari Salum, mwaka 2010 ndugu wa
mkewe aitwaye Nyasenene aliyekuwa akiishi Charambe Mbagala, jijini Dar
alifika nyumbani kwake na kuwaomba wampe mtoto wao kwa ajili ya kwenda
kufanya kazi za ndani ‘hausigeli’.
Mzee huyo amesema alikwenda Muhimbili na kufanikiwa kuzungumza
machache na mwanaye huyo ambapo alikuwa akilalamikia maumivu ya tumbo.
Mzee huyo alisema ilibidi aondoke licha ya mwanaye kumtaka alale
lakini kwa vile yeye ni mwanaume isingewezekana kulala hospitalini hapo.
“Kesho yake nilipewa taarifa kuwa mwanangu amefariki dunia usiku.
Tulianza taratibu za mazishi na kumzika kwenye Makaburi ya Kichangani,
Mbagala, Dar kutokana na kukosa fedha za kuusafirisha mwili hadi
Mkuranga,” alisema mzazi huyo
Mganga wa kienyeji aliyejulikana kwa jina la Said Ali Ngaora ‘Dr.
Lamba’ anayeishi Mbagala Rangi Tatu, Dar alifika katika kijiji hicho
cha Kalole mwaka huu na kuwaambia wananchi kuwa kijijini hapo pana mtu
anaonekana alikufa na kuzikwa lakini bado yupo hai na amewekwa sehemu na
kutaja gharama za kumtoa ni shilingi milioni tatu.
Akielezea tukio zima Dr. Lamba alisema wananchi walimruhusu akaanza kazi kwa kushirikiana na wataalamu wenzake.
Dr. Lamba na timu yake walifanikiwa kumuibua msichana huyo
anayekadiriwa kuwa na miaka 12-15 kwenye mji ambao hakuna mtu anayeishi
akiwa ndani ya banda la kuku huku kukiwa na chungu chenye damu, asali na
udongo ambavyo vilikuwa ndivyo vyakula vyake akiwa na muonekano wa
kutisha kwa kuwa na nywele ndefu na chafu na kucha zikiwa ndefu mithili
ya jini.
Baada ya kumtoa alipelekwa katika uwanja wa mpira kijijini hapo na
kuogeshwa pamoja na kukatwa kucha kisha akapelekwa katika nyumba
aliyofikia mganga huyo, hata hivyo hakuweza kuongea vizuri.
Kwa mujibu wa mashuhuda ulimi wa Nuru ulikuwa mzito na mpaka sasa
anazungumza kwa vitendo kama bubu huku chakula ambacho ameanza kula
vikiwa ni ugali na kuku, uji na juisi ya embe.
Mbali na shilingi milioni tatu za kutoa, mganga huyo anataka milioni
15 kutokana na dawa anazompa kwa ajili ya matibabu ili arudi katika
hali ya kibinadamu .
Hata hivyo, baadhi ya ndugu wanaopinga kuwa Nuru siyo mtoto wao
lakini baba mzazi anasema ni mwanaye kutokana na alama zilizopo
mgongoni mwake na anafanana sana na mdogo wake.
Makamu Mwenyekiti wa kijiji hicho,
Ali Hassan Ndeko alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema mpaka
sasa wanakijiji wanaendelea kumiminika kwa ajili ya kumuona mtoto huyo
akiwa chini ya uangalizi maalumu wa mganga huyo huku wakijitolea
vyakula.
GPL:
No comments:
Post a Comment