Blogger Widgets

July 16, 2013

Idadi Iliyoongezeka ya wanajeshi Wengine waliofariki Huko Sudani

WINGU zito limetanda kwa askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), katika nchi za Sudani Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Wakati Watanzania wakiendelea kuomboleza vifo vya wanajeshi saba wa jeshi hilo waliopoteza maisha katika Jimbo la Darfur, Sudani kwa kushambuliwa na waasi, nchini DRC yamezuka mapigano makali baina ya waasi na majeshi ya Serikali.

Mapigano hayo yameripotiwa kuibuka kati ya Wanajeshi wa Serikali na waasi karibu na mji wa Goma, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Msemaji wa wapiganaji wa waasi wa M23, ameliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kuwa ndege za kivita za Serikali zimefanya mashambulio ya anga katika maeneo yao usiku wa kuamkia jana.

Umoja wa mataifa kwa upande wake umesema uko tayari kutumia nguvu, kuwalinda raia ikiwa wapiganaji hao wa M23 wataingia katika mji wa Goma.

Raia wakimbia mapigano
Wakati huo huo, mashirika ya kutoa misaada ya kibinadamu, yamesema kuwa zaidi ya wakimbizi elfu sabini raia wa Congo wamekimbilia nchi jirani ya Uganda, kukwepa mapigano hayo.

Wapiganaji wa waasi wa Uganda nchini Congo, Allied Democratic Forces walishambulia mji wa Kamango na kusababisha mapigano makali kati yao na jeshi la serikali.

JWTZ: Askari wetu DRC wapo salama

Kwa upande wake, Msemaji wa Jeshi la Tanzania (JWTZ), Kanali Mgawe, alipoulizwa kuhusu mapigano hayo aliwataka wananchi kutokuwa na wasi wasi kuhusu usalama wa wanajeshi wa Tanzania.

“Wanajeshi wa Tanzania wapo salama hakijatokea kitu chochote tofauti na kama kuna tatizo lolote tutatoa taarifa, wanajeshi wetu nchini Kongo DRC wapo salama,” alisema.

Wanajeshi wengine wadaiwa kufa Darfur

WAKATI Watanzania wakiendelea kuomboleza vifo vya wanajeshi saba wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), waliokufa katika Jimbo la Darfur nchini Sudani, askari wengine watatu wa jeshi hilo wamedaiwa kupoteza maisha.

Idadi hiyo imedaiwa kuongezeka, baada ya wanajeshi hao watatu ambao ni kati ya 14 waliokuwa wamejeruhiwa vibaya, nao kupoteza maisha katika shambulizi la kushtukiza.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya JWTZ, kimesema kuwa askari hao wamefariki dunia baada ya jitihada za madaktari kuokoa maisha yao kushindikana.

Askari hao walifariki baada ya kushambuliwa na kikundi cha waasi wa Sudani, walipokuwa katika msafara wa kusindikiza waangalizi wa amani kutoka Khor Abeche kwenda Nyara, katika Jimbo la Darfur.

MTANZANIA ilipomtafuta msemaji wa jeshi hilo, Kanali Kapambala Mgawe kuzungumzia taarifa hizo, alisema hakuna taarifa zozote zinazoonesha kuwapo na ongezeko la idadi ya vifo vya Darfur, Sudani.

Kuhusu usafirishwaji wa miili ya askari hao kuja nchini, Kanali Mgawe alisema suala hilo la usafirishwaji wa miili ya askari hao, linaratibiwa na Umoja wa Mataifa (UN), ingawa JWTZ inafuatilia kwa karibu.

“Ninapenda kukuambia kuwa hadi sasa hakuna mwanajeshi aliyeongezeka, ila hizo ni taarifa ambazo si sahihi na zimekuwa zikienezwa katika mitandao ya kijamii. Sisi kama jeshi hatuna taarifa kama hizo,” alisema Kanali Mgawe.

Alipoulizwa kuhusu kutajwa kwa majina ya marehemu waliokufa katika tukio hilo la kushtukiza, Kanali Mgawe alisema jeshi haliwezi kutaja majina hayo kwa sasa, ila kinachofanyika ni kuwasiliana na ndugu wa marehemu hao.

“Safari hii asilimia kubwa ya askari wetu waliokwenda Sudan, wametoka katika mikoa ya mipakani, kwa hiyo tunachokifanya sasa tumeshawasiliana na makamanda wa kambi zote za jeshi ambazo wametoka marehemu hawa, ili waweze kuwasiliana na ndugu wa marehemu.

“Hivi ndugu utajisikiaje unasoma gazeti au unaangalia TV na kusikiliza redio halafu ukasikia kuwa ndugu yako amefariki utajisikiaje, ni lazima katika hili tuweze kufuata taratibu nzuri zinazokubalika kwa kuwasiliana nao moja kwa moja.

“Ninachotaka kuwahakikishia Watanzania kuwa JWTZ lipo imara na kama kuna taarifa yoyote tutaitoa mbele ya umma,” alisema.

Hata hivyo Kanali Mgawe alisema jeshi hilo limetuma ujumbe maalumu kwenda Darfur kuchunguza kiini cha tukio hilo, ingawa hakuweza kueleza kikosi hicho kinaundwa na wataalamu wa fani gani.

Read more: http://mwanahabariuswazi.blogspot.com/2013/07/wanajeshi-wengine-watatu-wa-tanzania.html#ixzz2ZCV7TWjF

No comments:

Post a Comment