ALI
Omar, mkazi wa Kijiji cha Mabana, wilayani Kilosa, Mkoa wa Morogoro
anashikiliwa na polisi kwa kosa la kumkata miguu Said Iddi kwa
kumtuhumu kumfumania na mkewe aliyejulikana kwa jina la mama Ali.
Tukio hilo la kikatili
lilijiri Julai 15, mwaka huu wakati Said na mama Ali walipokuwa ndani ya
nyumba ya Ali iliyopo kijijini hapo.
MANENO YA SHUHUDA
Akizungumza na mwandishi wetu,
shuhuda mmoja ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja alisema
Said alifumaniwa ndani ya nyumba asubuhi akiwa na mke wa Ali baada ya
kuwekewa mtego ambao ulimnasa vizuri.
“Ali alipewa habari na kijana
mmoja aitwaye God kwamba mkewe si mwaminifu katika ndoa, akamwongezea
kuwa anatoka kimapenzi na Said. Ndipo Ali na mnyetishaji wake huyo
walipopanga kumfumania jamaa,” alisema shuhuda.
Aliongeza kudai kuwa, Said ni
msimamizi wa mashamba ya Ali kijijini hapo na kwamba God ni mtoto wa
mwenye nyumba ambayo Ali amepanga kijijini hapo.
MPANGO WA FUMANIZI
Habari zinapasha kuwa mara
baada ya mnyetishaji kutoa taarifa za usaliti huo, Ali alimtafuta
‘baunsa’ ambaye jina lake halikuweza kujulikana mara moja na wakaweka
mtego kwa kujificha karibu na nyumba hiyo ambayo Said angeingia ili
kuivunja amri ya sita ya Mungu.
Katika kufanikisha mtego huo, mmbeya huyo alipewa jukumu la
kuhakikisha nyendo za Said na mama Ali siku hiyo zinarekodiwa mpaka
kuingia ndani ya nyumba hiyo na kumtaarifu Ali ambaye siku hiyo alimuaga
mkewe kwamba amesafiri.
SAID ATINGA NYUMBANI KWA ALI
Habari zinasema mtoboa siri huyo alimwambia Said kuwa Ali amesafiri
na ndipo jamaa akafunga safari kwenda kwa mama Ali kwa nia ya
kujivinjari licha ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ukifikia katikati.
Habari zinadai mara baada ya kufika kwa Ali, Said aliingia ndani ya
nyumba bila kujua kwamba mwenye mke alikuwa amejificha jirani akisubiri
mtego unase.
Inasemekana Said akiwa ndani, Ali na baunsa wake waliibuka kwa
kutaarifiwa na God na kumnasa jamaa huyo huku akidai ni mgoni wake.
Alimuuliza maswali kadhaa, yakiwemo haya:
“Umekuja kufanya nini ndani ya nyumba yangu? Kwa nini umekaa na mke wangu?”
Habari zinasema Said alijibu hakuona ubaya kwa kuwa yeye ni
mwangalizi wa mashamba ya mwanaume huyo hivyo anaweza kuingia ndani
kwake wakati wowote.
MWENYE MKE ATIBUKA NA MAJIBU, AMWAGA DAMU
Jibu hilo lilidaiwa kumtibua Ali na ndipo yeye na baunsa wake
wapomfunga kamba miguuni Said na kuanza kumkata kwa panga mguu mmoja
kisha kuugeukia wa pili.
Said alipiga mayowe yaliyowafanya wanakijiji kukimbilia eneo la tukio
kwa lengo la kujua kulikoni ambapo walimkuta Said akiwa anavuja damu na
sehemu ya nyuma ya miguu ikiwa nyanga’nyang’a.
MWENYE MKE AKIMBIA, ANASWA
Ali, God na baunsa walikimbia eneo hilo. Baadhi ya wanawake walitumia
khanga zao kuifunga miguu ya Said kwa lengo la kujaribu kuzuia damu
isiendelee kumwagika. Said alikuwa akilia sana.
“Wanakijiji walichukizwa sana na ukatili uliofanywa na Ali, hivyo
wakaanza kumsaka na kumkamata kichakani akiwa amejificha pamoja na God.
Alipewa mkong’oto kwa lengo la kutaka kumuua, lakini viongozi wa kijiji
walisihi asiuawe bali afikishwe kwenye kituo cha polisi,” alisema
shuhuda.
MKE, MUME, MMBEYA WAFIKISHWA POLISI
Polisi wa Kituo cha Dumila waliitwa na kumchukua Said, Ali na God kwa
kutumia gari aina ya Land Rover lenye namba za usajili T 750 AAJ. Mke
wa Ali yeye alipelekwa polisi kwa pikipiki.
Walipofika kituoni, Said alipewa fomu ya matibabu ya polisi (PF 3) na kupelekwa Hospitali ya Wilaya ya Kilosa kwa matibabu.
“Pale hospitali Said alishonwa miguu yote lakini madaktari wakaamua
ahamishiwe katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa matibabu zaidi,”
alisema shuhuda huyo.
ANAWEZA ASITEMBEE TENA
Akaongeza: Daktari mmoja alisema haamini kama jamaa (Said) atatembea
tena kwa sababu zana iliyotumika kumkata ilifika hadi kwenye mishipa ya
nyuma ambayo ndiyo humfanya binadamu aweze kusimama na kutembea.
BAUNSA ASAKWA
Afisa mmoja wa polisi kituoni hapo ambaye hakupenda jina lake
liandikwe kwa kuwa si msemaji, alisema wanaendelea kumsaka baunsa
aliyeshirikiana na Ali kumkata miguu Said.
-GPL
No comments:
Post a Comment