Blogger Widgets

July 15, 2013

Ukweli Juu Tetesi za Kunyongwa Kwa Model Binti Kiziwi Huko China

 
Mrembo aliyehukumiwa miaka mitano Sandra Khan 'Binti Kiziwi'.

MTANDAO wa wauza madawa ya kulevya unazidi kupukutika Bongo kufuatia madai ya kukamatwa kwa watu wanaodaiwa kujishughulisha na ubebaji ‘punda’ wa biashara hiyo haramu, Ijumaa Wikienda lina mtiririko wote.  Hivi karibuni, Video Queen wa Wimbo wa Masogange, Agnes Gerald ‘Masogange’ amedaiwa kunaswa nchini Afrika Kusini ‘Sauzi’ akiwa na kilo mia moja na hamsini za unga unaoaminika ni sehemu ya madawa ya kulevya. Ameshapanda kortini mara moja Ijumaa iliyopita.
Wakati Masogange akisota Sauzi kwa madai hayo mazito, habari ya mjini kwa sasa ni ya mtalaka wa mwanamuziki wa Bongo Fleva, Ally Mohammed ’Z-Anto’, Sandra Khan au Binti Kiziwi kudaiwa kutupwa jela miaka mitano kwa sakata la ‘unga’.

HABARI YA MJINI KWA SASA NI BINTI KIZIWI 
Kuanzia Alhamisi iliyopita, habari zilizoligubika Jiji la Dar ni kuwa Binti Kiziwi amenyongwa nchini China baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na madawa ya kulevya.
Kwa mujibu wa mitandao, Binti Kiziwi alinyongwa wiki mbili zilizopita.
Hata hivyo, mitandao hiyo haikusema kama mrembo huyo alinyongwa hadi kufa au la! Sheria za hukumu hiyo, mwenye hatia anatakiwa kunyongwa hadi kufa.

 
Agnes Gerald ‘Masogange’.

UKWELI WA BINTI KIZIWI NI HUU
Baada ya kusambaa kwa manenomaneno hayo, Ijumaa Wikienda liliingia mtaani kuisaka familia ya Binti Kiziwi lakini bila mafanikio. 
Kwenye makazi ya mama yake, Buguruni, Dar, majirani walisema mzazi huyo amehama baada ya kufunga ndoa siku chache kabla ya Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
 
IJUMAA WIKIENDA LAZIDI KUCHIMBA
Ijumaa Wikienda lilizidi kuzama ndani katika kuchimbua tetesi hizo ambapo lilifanikiwa kumpata ndugu wa kiume wa Binti Kiziwi na kufanya naye mazungumzo kama ifuatavyo:
Wikienda: Samahani, nimeambiwa wewe ni ndugu wa Binti Kiziwi, ni kweli?
Ndugu: (huku akitaja uhusiano wao) Ni kweli, nikusaidie nini?
Wikienda: Kuna manenomaneno kwamba Binti Kiziwi amenyongwa nchini China baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na madawa ya kulevya, ni kweli?
Ndugu: Sijui hizo habari watu wanazipatia wapi?! Watanzania wana maneno sana. Si kweli ndugu mwandishi.
Wikienda: Ukweli ni upi?
Ndugu: Kwanza kabisa Binti Kiziwi hakukamatiwa China, alikamatiwa Hong Kong, kwa sheria za kule mtu akipatikana na hatia ya kukutwa na ‘unga’ anahukumiwa jela tu.
“Binti Kiziwi amehukumiwa miaka mitano jela Hong Kong, na si China. Watu wajue hilo na miaka mitano si mingi, atatoka.”
Wikienda: Nashukuru sana kwa ushirikiano ndugu yangu.
Ndugu: Asante, waambie Watanzania waache kuongeaongea sana.

 
Saada Ally Kilongo (26), maarufu kama ‘Demu wa Kanumba’.

DEMU WA KANUMBA NAYE ASOTA RUMANDE
Msichana anayejulikana kwa jina la Saada Ally Kilongo (26), maarufu kama ‘Demu wa Kanumba’ yeye bado anasota kwenye Gereza la Segerea, Dar kwa tuhuma za kukutwa na madawa ya kulevya yanayokadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni 170.
Saada alidakwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar Juni 24, mwaka huu. 
Kesi yake ilisikilizwa kwa mara ya kwanza, Juni 29, mwaka huu kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu, Dar es Salaam.
Mdada huyo mkazi wa Mbezi Beach, Dar aliwahi kutoka kwenye Gazeti la Ijumaa la Desemba 9, 2011 ukurasa wa mbele kwa kichwa cha habari kisemacho: SAA 7 USIKU KANUMBA AGANDANA NA DEMU.
Demu huyo ambaye wakati huo alikuwa mwanafunzi wa Chuo cha Ustawi wa Jamii, Kijitonyama, Dar (alimaliza mwaka jana), picha yake akiwa na marehemu Kanumba ilipigwa Desemba 2, 2011 ndani ya Ukumbi wa Mlimani City, Dar ambapo kulirindima Tamasha la Usiku wa Kiafrika lililopambwa na mkali wa dansi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Ipupa Nsimba ‘Fally Ipupa’.

 
Sharifa Mahamoud (27).

MSANII BONGO MUVI ‘ASUBIRI KITANZI’ MISRI
Wakati mlolongo wote ukiwa hivyo, mrembo aliyewahi kushiriki filamu Bongo, Sharifa Mahamoud (27) naye anashikiliwa katika gereza moja nchini Misri wakati kesi yake ya kukamatwa na madawa ya kulevya ikirindima nchini humo.

BALOZI WA TANZANIA -MISRI AZUNGUMZA
Kwa mujibu wa Balozi wa Tanzania nchini Misri, Mohammed Haji, Mei 18, mwaka huu, Sharifa na nduguye, Abdallah Salum (28), wote wakazi wa Magomeni, Dar, walinaswa na unga jijini Cairo wakitokea Dar. 
Mei 26, walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza. Madawa waliokutwa nayo ni heroine kilo saba (gharama ya fedha haikutajwa). 
Kwa sheria za Misri, kosa la kukutwa na madawa ya kulevya ni kunyongwa hadi kufa. Lakini kwa mujibu wa Balozi Salum, hana kumbukumbu za raia wa kigeni aliyewahi kuhukumiwa kunyongwa nchini humo kwa kosa hilo.
Balozi alisema: “Endapo watapatikana na hatia kwamba kweli dawa hizo zilikuwa zao, hili litakuwa doa la kwanza kwa nchi yetu (Tanzania) hapa Misri.
Kwa mujibu wa Sharifa wakati akihojiwa na TV ya Misri, alishangaa kuona begi lake likiwa na madawa ya kulevya baada ya kukamatwa na kwamba aliingia nchini humo kumtafuta binamu yake.
From: GPL

No comments:

Post a Comment