Said Salim Awadh Bakhresa.
KATI ya
miaka ya 1960 hadi 1980, mtu kuwa tajiri alionekana ni hatari kwa taifa,
tena mali zake alizimiliki kwa kificho, vinginevyo angeitwa mhujumu
uchumi. Lakini kwa sasa mambo yamebadilika, taratibu sera za kibepari
zinatawala, ujamaa unapewa kisogo.
Mtu kama
ni mbunifu, ana nidhamu ya kutofuja pesa na anafanya kazi sana kwa nini
asiwe tajiri? Utandawazi unasaidia ndiyo maana leo tunaweza kuwatambua
mabilionea wakubwa ambao wanastahili pongezi kwa hatua walizopiga.
Tusisahau kuwa wanaibeba nchi kwa ulipaji kodi.Na Gpl
1. SAID BAKHRESA
Jina lake kamili ni Said Salim
Awadh Bakhresa. Jarida la Forbes mwaka jana, lilimuorodhesha miongoni
mwa matajiri 40 Afrika kwamba anamiliki utajiri wenye thamani ya dola
milioni 620 (karibu shilingi trilioni moja). Hata hivyo, inadaiwa kuwa
tabia ya usiri wa Bakhresa inafanya mali zake zisijulikane sana, ila ni
tajiri zaidi ya kiwango hicho.
Ndiye mmiliki wa makampuni ya
Bakhresa yanayotoa bidhaa zenye chapa ya Azam ambazo zinauzwa nchi
mbalimbali Afrika. Ana viwanda vya nafaka na vinywaji, vyombo vya
usafiri wa majini, uuzaji wa chakula, bidhaa za plastiki na kadhalika.
Ndiye mmiliki wa Klabu ya Azam FC.
2. GULAM DEWJI
Huyu
ni baba wa mfanyabiashara maarufu nchini, Mohamed Dewji ‘Mo’. Jarida la
Forbes mwaka jana lilimtaja kuwa na utajiri wenye thamani ya dola
milioni 560 (karibu shilingi bilioni 900). Mafanikio yake kibiashara
yalianza mwaka 1970. Kiwanda chake cha 21st Century Textiles, kinatajwa
kuwa moja ya viwanda vikubwa vya nguo Afrika.
3. ROSTAM AZIZ
Inadaiwa anamiliki utajiri
wenye thamani ya dola milioni 420 (shilingi bilioni 672). Anamiliki
karibu asilimia 40 ya hisa Kampuni ya Vodacom Tanzania. Ni mmiliki wa
Kampuni ya Caspian inayohusika na uchimbaji wa madini na ukandarasi
nchini Tanzania, nchi kadhaa za Afrika na Asia.
4. DK. REGINALD MENGI
Anatajwa kumiliki utajiri
wenye thamani ya dola milioni 280 (karibu shilingi bilioni 450). Ni
mmiliki wa kundi la makampuni ya IPP, yanayomiliki vyombo vya habari,
viwanda, migodi ya dhahabu, Tanzanite na kadhalika.
5. ALI MUFURUKI
Utajiri wake unatajwa kuwa na
thamani ya dola milioni 110 (shilingi bilioni 176). Ni mmiliki wa kundi
la makumpuni ya Infortech Investment, inayomiliki maduka yanayouza vitu
vya rejareja Tanzania na Uganda. Vilevile ana vitega uchumi vingine.
6. MUSTAFA SABODO
Ni mfayabiashara mkubwa sana
nchini anayemwaga mamilioni kwa misaada. Wakati wa kuanzishwa kwake,
aliipa Taasisi ya Mwalimu Nyerere shilingi milioni 800, akasaidia
shilingi milioni 100 katika mradi wa kustawisha mimea jamii ya kunde.
Vilevile alikipa Chadema shilingi milioni 300. Inadaiwa kuwa utajiri
wake unazidi shilingi bilioni 100. Kampuni yake ya Khoja Shia Itnasheri
Jamat (KSIJ), ndiyo yeye tenda ya kujenga maeneo ya maegesho ya magari
Posta, Dar es Salaam, mradi wenye thamani ya shilingi bilioni 5.6.
7. ABDUL-AZIZ ABOOD
Kiwango chake cha utajiri
hakiwekwi sana wazi lakini anatajwa kuwa miongoni mwa mabilionea 10
wanaotikisa nchi kwa sasa. Anamiliki viwanda kadhaa mkoani Morogoro,
vyombo vya habari, Abood Radio na TV. Anamiliki mabasi ambayo yanafanya
safari zake kati ya Morogoro, Mbeya na Dar es Salaam. Ni Mbunge wa
Morogoro Mjini (CCM).
8. MICHAEL SHIRIMA
Ni mmiliki mkuu wa Shirika la
Ndege la Precision ambalo linafaya safari zake ndani ya Tanzania pamoja
na nchi mbalimbali za Afrika. Ana asilimia tano ya hisa katika Beki ya
I&M (Tanzania), vilevile ni memba katika bodi ya wakurugenzi wa
benki hiyo yenye thamani ta shilingi bilioni 200. Hisa zake Precision ni
asilimia 42.91.
9. YUSUF MANJI
Kiwango halisi cha utajiri
wake bado hakifahamiki lakini anafahamika kama mmoja wa mabilionea
wakubwa nchini Tanzania. Ni mmiliki wa makampuni ya Quality Group na
majengo ya Quality Centre, Quality Plaza na kadhalika. Ni Mwenyekiti wa
Klabu ya Yanga na utajiri wake umeifaya timu kutotetereka tangu
alipoanza kuiongoza.
10. MOHAMMED DEWJI
Baba yake anashika nafasi ya
pili katika orodha hii. Dewji au Mo kama anavyoitwa na wengi, anatajwa
kuwa bilionea nambari moja katika orodha ya mabilionea vijana Afrika
(orodha hiyo tuliitoa wiki iliyopita). Ni mmiliki wa makampuni ya
Mohammed Enterprises Tanzania Limited (METL) ambayo inatengeneza faida
ya shilingi bilioni 136 kwa mwaka.
No comments:
Post a Comment