JESHI
la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limemkamata Saida Mohamed
(30), mkazi wa Mwasonga Kigamboni, akiwa na sare za Jeshi la Wananchi
Tanzania (JWTZ).
Akizungumza
na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamishna wa Polisi Kanda
Maalum ya Dar es Salaam, Suleimani Kova, alisema mtuhumiwa huyo
alikamatwa Agosti 31, mwaka huu, katika eneo la Mwasonga, Kigamboni.
Alisema
Saida alikamatwa na suruali saba, mashati saba ya kombati, kofia 10,
shati mbili nyepesi, fulana mbili na kofia moja aina ya bareti, vyote
vikiwa mali ya JWTZ.
Alisema mtuhumiwa huyo, alikuwa na begi moja la kuwekea nguo za jeshi, cheo kimoja cha Koplo na mikanda miwili ya kijeshi.
Alisema uchunguzi unaendelea juu ya mwanamke huyo ili kubaini sababu za kumiliki sare za jeshi, kabla ya kufikishwa mahakamani.
Katika
tukio jingine, polisi wamemkamata Husein Mkondoa (25), mkazi wa
Gongolamboto Mzambarauni, akiwa anaendesha pikipiki huku akiwa amevaa
nguo za kiraia na kofia ngumu ya kijani yenye nembo ya Polisi.
Alisema polisi walimtilia mashaka na kumkamata mtuhumiwa na anaendelea kuhojiwa.
“Naomba
kutoa onyo kwa watu wote wenye silaha na sare za jeshi wazisalimishe
kwa polisi au ofisi yoyote ya Serikali, msako wa kuwakamata wahalifu
utakuwa endelevu na tutaingia nyumba hadi nyumba kuwatafuta wahalifu.
“Sambamba
na operesheni hii, licha ya kubadilisha uongozi katika kituo cha Polisi
Ubungo, tumeamua kutupia macho vitendo vya utapeli katika eneo la
Ubungo Bus Terminal, ambalo watu wengi wanajifanya askari.
“Licha
ya hilo, tumeunda kikosi cha kutumia video kamera na kamera za picha
mnato ili kubaini na kuchukua hatua na nyendo mbalimbali ili kujenga
ushahidi wa wahalifu hao wasiepuke mkono wa sheria,” alisema Kova.
Wakati
huo huo, Jeshi la Polisi linawashikilia watuhumiwa wawili kwa kuchonga
hati mbalimbali zinazotaka kufanana na za Serikali.
Kamishina
Kova, aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Shadrack Samwel (27) mkazi wa
Mbagala Sabasaba na Mwangi Samwel (38) mkazi wa Kimara Baruti.
Alisema
watu hao, hawana ofisi maalumu hivyo hufanya shughuli hiyo sehemu
yoyote na ofisi zao kuu ni mkoba pamoja na gari ambalo wanatembelea,
lenye namba za usajili T 397 ADX aina ya Crester.
“Watuhumiwa
hawa, tuliwakuta na mihuri 27 ambayo ni ya Serikali na taasisi binafsi,
mihuri ya mawakili wa kujitegemea na wa serikalini, mhuri wa Jeshi
pamoja na mhuri wa Serikali za mitaa.
“Pia
tumewakamata na nakala mbalimbali za SUMATRA, ikiwemo karatasi za
kukagulia magari, pleti namba za magari pamoja na nakala mbalimbali za
ofisi hiyo,” alisema.
Katika
hatua nyingine, polisi wanawashikilia watu watano, akiwamo Enea
Dawsoni, ambaye ni mfanyakazi katika Kapuni ya Ndege ya Fast Jet, kwa
jaribio la kutaka kupora fedha kiasi cha Sh 60,000,000 katika Kampuni
hiyo.
Alisema watuhumiwa hao walinaswa katika Mtaa wa Samora na iligundulika walikuwa wana mawasiliano ya simu.
“Baada
ya kuwakamata watu hawa, Polisi walielekea katika ofisi hizo na baada
ya kufika walichukua simu ya watuhumiwa hao na kuona ujumbe mfupi wa
maneno, ulioeleza kuwa fedha zipo karibu na chooni.
“Polisi
walichukua simu ya wahalifu na walipopiga simu hiyo iliyokuwa na
mawasiliano na majambazi hao, simu iliita kwa sauti kubwa ndani ya
maungo ya mmoja kati ya watumishi wa Fast Jet.
“Mtumishi
Enea Dawson alikuwa ameficha simu hiyo sehemu za siri katika nguo zake
ambapo aliumbuka na kugundulika kuwa alikuwa na uhusiano wa karibu na
majambazi hao,” alisema Kova.
Soma zaidi: http://mwanahabariuswazi.blogspot.com/2013/09/mwanamke-atiwa-mbaroni-baada-ya-kunaswa.html#ixzz2dpBy3eSz
No comments:
Post a Comment