Blogger Widgets

September 3, 2013

Tazama Picha za Vigogo waliokamatwa na Shehena ya Madawa ya Kulenya Yenye Thamani ya Sh. Billion 6.2



  VITA dhidi ya biashara ya madawa ya kulevya ni ngumu sana, dirisha la mafanikio ya kudhibiti linafungwa na vigogo wauza unga ambao wana fedha nyingi zinazoyumbisha sheria kuchukua mkondo wake.

Pointi nambari moja ni uwepo wa ripoti za ukamatwaji wauza unga lakini hukumu hazitolewi, swali kwa nini hawahukumiwi likipashwa moto ili kuunguza mamlaka zinazohusika, Uwazi linafichua siri nzito kuhusu madai ya vigogo waliokamatwa na kuachiwa.

Watu wanne ambao wanatajwa kuwa miongoni mwa vinara wa madawa ya kulevya nchini, walikamatwa na madawa ya kulevya yenye thamani ya shilingi bilioni 6.2 kisha wakafikishwa mahakamani ambako inadaiwa wameachiwa katika mazingira tatanishi.

 

Abdul.

Vigogo hao wanne, wapo Watanzania wawili na wengine ni raia wa Pakistan ambao sasa hivi inadaiwa wameshatoroka kwenda nje ya nchi.

MCHEZO ULIKUWAJE?

Februari 21, 2011, jeshi la polisi kupitia kitengo cha kudhibiti na kupambana na madawa ya kulevya, kiliwakamata wafanyabiashara hao ambao majina yao ni William Chonde na Kambi Zuberi (Watanzania) pamoja na Wapakistan, Abdul Ghan Peer Bux na Shahbaz Malk.

 

Kambi.

Watu hao, walikamatwa na mzigo huo Mbezi Jogoo, Dar es Salaam kwenye nyumba ya Chonde, wakiwa na madawa ya kulevya aina ya heroine, yenye uzito wa kilo 179 ambayo thamani yake ni shilingi 6,265,000,000.

Sera ya Uwazi ni kuendeleza safari iliyoianzisha kwa vile ndilo liliandika pale walipokamatwa zaidi ya miaka miwili iliyopita. Wiki mbili zilizopita, lilianza upekuzi kujua kesi hiyo imefikia wapi.

Uchunguzi wa waandishi wetu uliweza kubaini kuwa watuhumiwa hao wa madawa ya kulevya waliachiwa na mahakama kuu kwa dhamana, kinyume na sheria ya madawa ya kulevya inavyoeleza.

 

Shahbaz.

SHERIA INASEMAJE?

Sheria ya madawa ya kulevya ya mwaka 1996, sura ya 95, kipengele nambari 9, kifungu nambari 27, kifungu kidogo nambari 1A, kinasema: “Yeyote atakayekamatwa na madawa ya kulevya yenye thamani zaidi ya shilingi milioni 10 hapaswi kupewa dhamana.”

Vilevile, sheria hiyo inaendelea katika kifungu kidogo nambari 1B ambacho kinasema: “Yeyote atakayekamatwa akisafirisha madawa ya kulevya hapaswi kudhaminiwa.”

 

Fred.

KAMANDA MADAWA YA KULEVYA ALIA

Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti na Kupambana na Madawa ya Kulevya Tanzania, Godfrey Nzowa, alipoulizwa kuhusu kile anachokifahamu kufuatia kuachiwa kwa watuhumiwa hao, alijibu:

“Mimi sijui, waliachiwa mahakamani. Kazi yetu sisi ilikuwa ni kuwakamata, kila kitu kikapelekwa kwa DPP (mkurugenzi wa mashtaka), baada ya hapo kesi ilikwenda kwa msajili wa mahakama.

Nijuavyo mimi ni kwamba walifikishwa mahakamani na nilisikia waliachiwa kwa dhamana,” alisema Nzowa.

Kamanda Nzowa.

KWA NINI WATUHUMIWA WALIACHIWA NA KUPEWA HATI ZA KUSAFIRIA?

Yapo madai kwamba baada ya watuhumiwa hao kupewa dhamana, walikabidhiwa hati za kusafiria (passport) ambazo ziliwawezesha kutoroka. Uwazi lambana Nzowa;

UWAZI: Unaweza kufahamu kigezo kipi kilitumika kuwapa dhamana watuhumiwa hao? Maana sheria inakataza.

NZOWA: Nadhani mahakama ndiyo inapaswa kuulizwa swali hilo. Siwezi kuisemea, maana ule ni mhimili mwingine huru.

UWAZI: Inadaiwa wewe ndiye uliwapa passport zao na sasa tunaambiwa walishatoroka nchini, hili limekaaje?

NZOWA: Ni kweli tuliwapa passport zao, tuliagizwa na mahakama kufanya hivyo.

MSAJILI WA MAHAKAMA KUU

Msajili wa Mahakama Kuu, Benedict Mwingwa, alipoulizwa kuhusu kuachiwa kwa watuhumiwa hao kwa dhamana, aling’aka, kisha akaahidi kufuatilia kujua kisa na mkasa.

“Nimeshtushwa sana na hilo jambo. Ni kweli sheria inakataza, sasa watuhumiwa kama hao hawakupaswa kudhaminiwa. Nalifanyia kazi, nitakutana na jaji anayesikiliza kesi hiyo aniambie sheria aliyotumia,” alisema Mwingwa.

MOTO UNAWAKA

Uchunguzi wa Uwazi umebaini kwamba baada ya malalamiko ya muda mrefu kuhusu kusuasua kwa kesi za madawa ya kulevya ambayo yanaelekezwa Mahakama Kuu, Jaji Kiongozi, Fakhi Jundu, aliitisha mkutano wa dharura wiki mbili zilizopita.

Mkutano huo ulishirikisha majaji wa mahakama kuu, idara ya usalama wa taifa, Takukuru, ofisi ya DPP, mkemia mkuu wa serikali, magereza, polisi na kitengo cha kudhibiti na kupambana na madawa ya kulevya.

Vyanzo vyetu vinasema kuwa katika mkutano huo, maazimio ya pamoja ni kila idara kutimiza wajibu wake bila kutazama sura wala nafasi ya mtu ili haki ionekane ikitendeka, huku ikisisitizwa kesi kuharakishwa na hukumu kutolewa.

UWAZI LIPO KAZINI

Gazeti hili linaendelea kutenda kazi yake. Linaahidi kufuatilia kesi nyingine zaidi na litaziweka wazi kulingana na ukweli wake. Tunafahamu kwamba kesi ni nyingi, watuhumiwa ni wengi lakini hukumu hazitolewi.

From:Uwazi

No comments:

Post a Comment