Blogger Widgets

October 30, 2013

Tazama Jeneza La Diamond Platnum Lililozua Utata


STAA wa muziki wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’ ambaye hakaukiwi na stori, safari hii amekuja na mpya baada ya kuibuka na jeneza lenye msalaba ambalo limeibua maswali mazito, Risasi Mchanganyiko linakupasha.

Diamond akipozi na madansa wake siku alipoingia na jeneza katika Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni, Dar.
Diamond ambaye wimbo wake mpya wa ‘Number One’ upo katika chati ya juu katika muziki huo, usiku wa kuamkia Jumapili iliyopita aliingia na jeneza hilo katika Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni, Dar na kusababisha maswali mengi tata kutoka kwa mashabiki waliojazana kwenye onesho la Serengeti Fiesta 2013.
ILIKUWA SAPRAIZI
Mapaparazi wa Risasi Mchanganyiko waliokuwa wamejaa katika viwanja hivyo wakihakikisha wananasa matukio muhimu hasa yale ‘exclusive’, walipenyezewa mapema kuhusu Diamond kuingia na jeneza.

Mtoa habari alisema Diamond aliingiza jeneza viwanjani humo kwa lengo la kupanda nalo jukwaani wakati akiimba wimbo wake uitwao Nikifa Kesho ambao mashabiki wake wengi wanasema amejichulia kifo.

Kwa sharti la kutoandikwa jina lake gazetini, mtoa habari huyo ambaye ni mtu wa karibu na Diamond alisema:
“Diamond amekuja na jeneza, limefichwa kule nyuma wanakobadilishia nguo wasanii, atapanda nalo jukwaani. Anataka kuwafanyia sapraizi mashabiki wake.”

Diamond akifanya shoo na madensa wake Jumapili iliyopita baada ya kutelekeza jeneza lake.

SAPRAIZI YAKWAMA
Hata hivyo, baada ya matatizo ya kiufundi yaliyojitokeza, Diamond hakuweza kupanda jukwaani Jumamosi usiku huo na badala yake akatakiwa kupanda kesho yake Jumapili ambapo pia hakulitumia jeneza hilo kama mawazo yake ya awali yalivyokuwa.
Mapaparazi wetu walisaka sehemu lilipohifadhiwa jeneza hilo na kufanikiwa ambapo pia walikuta baadhi ya watu wakilishangaa na kuulizana maswali.

MASWALI TATA
Nurdin Ali, mkazi wa Mbagala, Dar aliyeliona jeneza la Diamond alisema:
“Mimi namkubali sana huyu bwana mdogo lakini sasa mambo ya majeneza jukwaani ya nini tena?

“Sikubaliani na hili suala. Hata wimbo wake wa Nikifa Kesho sioni kama una mantiki. Ni kama tu anajitabiria kifo. Anapita mlemle alimopita marehemu Kanumba, maana naye aliimba wimbo akielezea itakavyokuwa siku akifa, ikawa kweli.
“Lakini Diamond amekwenda mbele zaidi kwa kuamua kuja na jeneza kabisa stejini. Sijui amenunua au amekodisha, ila sikubaliani naye hata kidogo.”

MATUMIZI YA JENEZA
Mwingine aliyekataa kuandikwa jina lake gazetini alisema:
“Halafu kama lengo lake lilikuwa kuonesha uhalisia wa kifo katika wimbo wake, kwa nini asingekuja na jeneza la imani yake? Angalia, jeneza lina msalaba ambao unakubalika katika imani ya Kikristo, kwa nini asije na jeneza la Kiislamu au sanduku ambalo halina msalaba?”

Akaongeza: Au inawezekana huyu jamaa anataka kubadili dini ili aoane na Penny (Penniel Mungilwa) ambaye ni Mkristo kwa sababu huku ni kukana imani yake kimyakimya.”

ALIWAHI KUTANGAZA KUJENGA MSIKITI
Shabiki mwingine alikwenda mbali zaidi na kusema kama Diamond ni muumini mzuri wa Kiislamu tena mwenye lengo la kujenga msikiti kama alivyowahi kutangaza siku za nyuma, anatakiwa kutofungamana kabisa na ishara zinazoonesha anaunga mkono imani nyingine.

“Anapaswa kuwa makini na mambo yake na awe na washauri wazuri, vinginevyo atakuwa anafanya mambo yanayoibua maswali mengi kwa jamii inayomwamini,” alisema shabiki huyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Jennifer.

HUYU YUPO TOFAUTI
Shabiki aliyejitambulisha kwa jina la Hamadi Hajj (34) mkazi wa Kijitonyama, Dar alisema:
“Hakuna uhusiano wowote kati ya hili jeneza na mambo ya kubadilisha dini au kuiunga mkono. Kikubwa ni lengo alilotaka litimie.
“Ukiachana na hilo, mambo mengine yako wazi jamani. Upatikanaji wa majeneza ya Kikristo ni rahisi zaidi tofauti na ya Kiislamu. Wabongo wanapenda sana kukuza mambo,”  alisema Hajj.

HUKU RISASI, KULE DIAMOND
Siku hiyohiyo, usiku huohuo, mapaparazi wetu walimbana Diamond kuhusu kutinga Leaders na jeneza ambapo alijitetea hivi:
“Ni swaga tu zile.”
Alipobanwa zaidi na kuulizwa ni swaga gani zinazochanganywa na vitu vinavyoashiria huzuni na imani ambayo si yake, alisema:
“Nilitaka kuwafurahisha mashabiki wangu na kuwapa uhalisia wa ule wimbo wangu wa Nikifa Kesho, sikuwa na nia ya kukashifu imani ya mtu.”

FIESTA PART II
Baada ya shoo yake kushindikana na kuhamishiwa siku iliyofuata (Jumapili), timu yetu ilitinga viwanjani hapo ili kujua kama Diamond angepanda na jeneza hilo kama alivyotarajia lakini jeneza halikuwepo eneo lilipohifadhiwa awali.
Diamond alipofuatwa na kuulizwa kama mpango wake bado uko palepale, alijibu:

“Lile jeneza nilipanga kupanda nalo jukwaani wakati nikiwa naimba wimbo wangu wa Nikifa Kesho lakini kwa bahati mbaya sikuweza kupanda kuimba kutokana na matatizo ya kiufundi, leo (Jumapili) nisingeweza kupanda nalo kwa kuwa muda tuliopewa ni mfupi sana,” alisema Diamond.

Alipobanwa kuhusu kutumia jeneza la Kikristo na kuhusishwa na fununu za kubadili dini, alisema hana mpango huo kabisa.
“Naomba nieleweke, mimi sikuwa na nia tofauti zaidi ya kuwakilisha kilichopo katika wimbo wangu. Lengo lilikuwa kuonesha uhalisia tu wa kibao changu cha Nikifa Kesho, siyo zaidi ya hivyo,” alisema.

Inasemekana kwamba Diamond aliamua kubadilisha uamuzi wake wa kupanda na jeneza jukwaani siku hiyo baada ya kunyetishwa na watu wanaomtakia mema kuwa asingeonesha picha nzuri kwa jamii, hasa kwa vile jeneza hilo lilikuwa na msalaba juu ya mfuniko.

katika Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni, Dar

No comments:

Post a Comment