Blogger Widgets

November 23, 2013

Taarifa Kamili ya Kuugua Ghafla kwa Mzee Gurumo na Kulazwa Hospitali ya Muhimbili

GWIJI wamuziki wa dansi, Muhidin Maalim Gurumo ameugua ghafla mapema leo na kulazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Wajumbe wa Kamati ya maandalizi ya Tamasha la Gurumo, Juma Mbizo na Said Mdoe, waliokuwepo Muhimbili, wameuambia mtandao huu kuwa mwimbaji huyo mkongwe alipatwa na tatizo la shinikizo la damu na hali ikawa mbaya kabla ya kukimbizwa hospitalini hapo.
Wamesema kwa sasa haliyake inaendelea vizuri na amelazwa katika wodi ya Mwaisela namba 1.
Wajumbe hao wamesema siku chache zilizopita, Gurumo alikuwa kwenye afya njema na hata siku ya Jumanne alihudhuria kikao cha kamati hiyo kilicho fanyika Vijana Social Hall Kinondoni.
Aidha, wajumbe hao wamedai kuwa kwamujibu wa mke wa Gurumo, Bi Pili, ni kwamba hata jana amwimbaji huyo alikuwa hana tatizo lolote na alifanya mizunguko yake bila ya mikwaruzo yoyote.
Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya tamasha la Gurumo, Bi Asha Baraka amewataka wapenzi wa muziki kuwa watulivu kwa vile hali ya mwanamuziki huyo aliyeitumikia fani kwa miaka 53, inaendelea vizuri.
Tamasha la Gurumo limepangwa kufanyika tarehe 14 mwezi ujao katika viwanja vya TCC Club Chang’ombe.
Tumuombee dua mzee wetu Gurumo.