Blogger Widgets

December 13, 2013

Msanii wa Kike wa Bongo Movie Coletha Aja Na Mpya


 
Coletha Raymond.
KUNA mambo mengine ni vigumu kufikiri kama yanaweza, siyo tu kutamkwa, bali kutendwa na mtu anayetegemewa na jamii kama mmoja wa vioo vyake. Kama ambavyo nimekuwa nikisema siku zote, watu maarufu wanaotokana na sanaa, wanastahili kuwa mfano.
Nimesema watu maarufu wanaotokana na sanaa, maana tunao baadhi ya wenzetu wana majina makubwa sana na yanayotamkwa kila mara ndani ya jamii yetu, lakini wakiwa na sifa zisizofaa. Wengine wanatambulika kwa ujambazi, uhusiano wa jinsia moja, utapeli na kadhalika. Hawa siyo mastaa ninaowalenga!
Mastaa, kwa maana ya wacheza filamu, wanasoka, wanamuziki na hata wanasiasa, wanapaswa kuwa makini sana kwa kila jambo wanalolisema na hata kulifanya.
Neno lao lolote, linachukuliwa kwa uzito wa aina yake mtaani, kwa sababu tu wao ni watu wa aina yake katika jamii yetu.
Siku kadhaa zilizopita nilikutana na habari ya huyu binti, mcheza filamu Coletha Raymond. Katika habari hiyo iliyoandikwa gazetini, msanii huyo alisema baada ya kutendwa na mwanaume wake wa zamani, sasa hahitaji tena kidume kingine, badala yake, anajikita katika unywaji wa pombe, kwa kile alichosema, kinampunguzia sana hamu ya ku-duu!

Coletha, kama nilivyosema, ni staa, msanii mwenye mashabiki wanaopenda sanaa anayoifanya. Kitu kimoja amewafundisha mashabiki wake, hasa watoto, kuwa kumbe pombe inaweza kumuondolea mtu hamu ya kupenda kushiriki tendo la ndoa!

Huu ni utani, tena mbaya. Sina uhakika na utafiti wa kitaalamu kuhusu pombe, lakini uzoefu unaonyesha watu wengi hujikuta wakifanya vitendo vya aibu, ikiwemo ngono zembe, baada ya kufakamia kinywaji.

Maneno haya yana tafsiri nyingi, hasa kama ni mtu unayefuatilia sana habari za mastaa wa Kibongo, hasa waigizaji kama Coletha na wale wa Bongo Fleva. Mojawapo ya ujumbe ambao mtu anaweza kuupata kwa kusikiliza kauli hii, ni kwamba msichana huyu hana mtu na kama atakuwa naye, basi si wa kudumu.
Pombe ni starehe lakini yenye gharama kubwa, kifedha na kimatokeo. Mtu anaweza kunywa pombe ya fedha kidogo, lakini akajikuta akiigharamia kwa kiasi kikubwa cha pesa kutokana na kile kinachotokana na huo ulabu aliopiga.
Anaweza akatukana watu, akafanya fujo zinazoweza kusababisha uharibifu mkubwa wa mali na vitendo vyake visivyo na tahadhari kutokana na pombe, vinaweza kusababisha tukio lolote baya.

Kwa Coletha kuiambia jamii kuwa anaichukulia pombe kama mbadala wa wanaume, ni jambo gumu kidogo kulielewa kwa haraka. Ni kweli, katika unywaji wa pombe, watu wametofautiana. Wapo ambao baada ya kupata, hutamani kushiriki tendo la ndoa (na hawa ni wengi), wengine huwa wazungumzaji sana na baadhi yao, hugeuka kuwa wakimya na wenye aibu.
Sijui kundi alilopo huyu mdada, ingawa uzoefu unaonyesha kuwa mastaa wetu wengi wanaokunywa pombe hushiriki mambo yetu yale.
Hata hivyo, kuhamasisha unywaji pombe, kama mbadala wa kitu chochote, siyo ushauri mzuri kutolewa kwa jamii kama yetu, ambayo imezungukwa na umasikini mkubwa. Huenda Coletha anao uwezo wa kuhimili vishindo vya kinywaji, lakini kwa wale wenzangu na mimi, hili linaweza kuwaongezea tatizo zaidi badala ya kuwapunguzia.
Coletha angeweza kunyamaza, lakini kama alilazimika kusema sababu za kutohitaji mwanaume baada ya kutendwa, mazoezi lilikuwa ni jibu zuri zaidi linaloweza kumsaidia mtu kupunguza hamu ya kushiriki tendo la ndoa.
Kama ninavyosema mara zote, mastaa wetu wanao wajibu mkubwa wa kuisaidia jamii yetu yenye mambo mengi. Kuisaidia siyo kwenda katika vituo vya watoto yatima na watu wasiojiweza na kupeleka sabuni na pipi, bali kupitia kauli na matendo yao.