Blogger Widgets

January 2, 2014

Mchungaji Peter Msigwa asisitiza kuwa Zitto Kabwe ni lazima avuliwe uanachama wa CHADEMA kesho

MBUNGE wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) ametaka wana Chadema kuunga mkono mpango wa kumfuta uanachama aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wao, Kabwe Zitto.
“Kuna mlolongo wa mambo yaliyofanya Chadema ikachukua hatua kali dhidi ya Zitto, mambo hayo yamesemwa sana na viongozi wetu; Januari 3, vikao vya chama vitaanza mchakato wa kuhitimisha suala hilo,” alisema.

 “Amekwishaandikiwa barua ya kujieleza kwa nini asifukuzwe uanachama, sasa nawaulizeni wana Chadema Iringa afukuzwe au asifukuzwe ili nikifika kwenye kikao nitoe msimamo wa Iringa?” Aliuliza na sehemu ya wananchi waliohudhuria mkutano wake wakijibu “afukuzweeee….”
 
Katika mkutano wake Desemba 31, kwenye Uwanja wa Mwembetogwa mjini hapa, Mchungaji Msigwa alisema Zitto amekikosea mengi chama hicho, hali iliyowanyima uvumilivu na kuamua kumwondoa katika nafasi zake zote za uongozi.
 
Alisema pamoja na kwamba alijiunga katika chama hicho akiwa na miaka 16, umaarufu wake kisiasa umechangiwa kwa kiasi kikubwa na waasisi wa chama hicho, aki wamo Mwenyekiti Freeman Mbowe aliyekuwa akimsaidia kifedha wakati akisoma Chuo Kikuu (cha Dar es Salaam).
 
Msigwa aliwasifu baadhi ya watendaji wa Serikali, akisema wanastahili pongezi kwa kazi nzuri wanayofanya kuwaletea wananchi maendeleo.
 
“Lazima tuwe waungwana, inapotokea kuna kazi imefanywa na watendaji, ni lazima tuwapongeze bila kujali wanaitumikia serikali ya chama gani,” alisema.
 
Alitaja watendaji hao kuwa ni Mkuu wa Mkoa, Dk Christine Ishengoma, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Dk Leticia Warioba na Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe.
 
Aliwapongeza viongozi hao kwa kukataa stendi mpya ya mabasi ijengwe Igumbilo, pembeni mwa Mto Ruaha Mdogo.
 
“Najua kuna watu walinunua viwanja kuzunguka stendi hiyo kwa gharama kubwa; na wameniandikia barua wakinitisha, kwamba hawataiunga mkono Chadema endapo nitaunga mkono stendi hiyo isijengwe pembeni mwa Mto huo,” alisema.
 
Alisema watu wanaotaka alifumbie macho suala la ujenzi wa stendi hiyo karibu na chanzo hicho cha maji ni bora waondoke Chadema kuliko kuwaunga mkono.
 
“Mbali na shughuli za kilimo, maji ya Mto huo ndio chanzo kikuu cha maji yanayotumika majumbani na wakazi wa Iringa na vitongoji vyake; ikijengwa stendi katika eneo hilo kutakuwa na uharibifu wa chanzo hicho unaoweza kuleta madhara kwenye maji ya Mto; sikubali, bora mtoke Chadema na kura zenu msinipe,” alisema.