Blogger Widgets

January 11, 2014

PICHA:Wananchi wa Kenya wameshangazwa na taarifa ya kuzinduka kwa mwanaume mmoja aliyedhaniwa kuwa amekufa ambapo alizinduka akiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya Naivasha

Hii ni kutoka kwa majirani zetu ambapo tunaambiwa Wananchi wa Kenya wameshangazwa na taarifa ya kuzinduka kwa mwanaume mmoja aliyedhaniwa kuwa amekufa ambapo alizinduka akiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali moja mjini Naivasha umbali wa kilomita tisini kutoka mji mkuu wa Kenya Nairobi.
Jamaa huyo anaitwa Paul Mburu ana umri wa miaka 24 ambapo alipelekwa hospitalini kwa matibabu baada ya kunywa sumu kwa lengo la kujitoa uhai kutokana na ugomvi wa kifamilia na babake ingawa ilisemekana jamaa alifariki  Jumatano usiku wakati akipokea matibabu.
Wafanyakazi wa hospitali hiyo walipigwa na butwaa na wengine kukimbia walipoona mwili wa mtu aliyedhaniwa kufariki ukitembea na kuonyesha dalili za kuwa hai katika chumba cha kuhifadhia maiti.
Afisa mkuu wa matibabu katika hospitali hiyo ya wilaya Dokta Joseph Mburu amesema kuwa dawa iliyotumiwa kumtibu Mburu hufanya moyo kupiga polepole hali ambayo huenda ilimfanya muuguzi kudhani kuwa mgonjwa alikua amefariki.
Raia huyo wa Kenya alisikika akimtaka mmoja wa wafanyakazi katika chumba cha kuhifadhia maiti kumsaidia kwani alikuwa anahisi baridi kali na hapo ndipo mmoja wa wafanyakazi alipotimua mbio kwa hofu.
Ndugu wa jamaa huyo akiwemo babake walikuwa wametembelea chumba cha kuhifadhia maiti siku ya Alhamisi ili kuanza kwa taratibu za mazishi lakini baadaye mchana walifahamishwa kuwa Mburu alikuwa hai.
Mgonjwa anaendelea kupokea matibabu katika hospitali ya Naivasha.

No comments:

Post a Comment