Blogger Widgets

February 8, 2014

Tazama Ushoga wa Dr.Cheni Ulivyomponza..

SIKU chache baada ya Bodi ya Filamu Tanzania (TFB) kuzuia filamu ya mkongwe katika sinema za Kibongo, Mahsein Awadh Said ‘Dk. Cheni’ ijulikanayo kwa jina la Nimekubali isiingie sokoni kwa madai kuwa imekiuka maadili ya Kitanzania, msanii huyo ameibuka na kueleza kinagaubaga, Risasi Jumamosi limenasa sauti yake.
Akizungumza na mwandishi wetu Jumatano ya wiki hii maeneo ya Mlimani City jijini Dar, msanii huyo alisema amesikitishwa na maamuzi ya bodi hiyo huku akidai kuwa lengo la filamu hiyo ni kukemea tabia za kishoga zinazoendelea kuibuka kwa vijana ikiwa ni pamoja na kupinga uhalali wa ndoa za jinsia moja.
Mkongwe wa sinema za Kibongo, Mahsein Awadh Said ‘Dk. Cheni’.
Katika maelezo hayo, DK. Cheni ambaye huzitendea haki filamu zake kwa kuvaa uhusika halisi, alisema moja ya kigezo ambacho bodi hiyo imekitumia kuzuia filamu hiyo ni pamoja na muonekano wa bango la filamu hiyo ambalo linamuonesha msanii huyo akiwa amevaa vazi la shera huku akiwa amejiremba kwa madai kuwa ni kuchochea ushoga jambo ambalo msanii huyo amelipinga vibaya.
“Eti ushoga wangu uko kwenye kujiremba sana, hakika wamenionea sana, lengo letu ni kuonya na kukemea vikali vitendo vya ushoga na ndoa za jinsia moja, huwezi kuelimisha bila kuonesha madhara yake kwa vitendo kama ilivyo ndani ya filamu hiyo.
Mkurugenzi wa bodi ya filamu,  Joyce Fissoo.
“Lakini, ndani ya filamu hiyo, kuna kipande ambacho kinaonesha kiongozi wa serikali akikemea kitendo hicho, sasa hapo ushoga wangu uko wapi? Kuvalia shera kwenye kava? Siyo sahihi,” alisema Dk. Cheni.
Mbali na kava hilo, msanii huyo alidai haoni kosa lolote katika filamu hiyo hivyo ataendelea kupigania haki yake na kwamba hayuko tayari kuonewa.
Jitihada za kumpa mkurugenzi wa bodi ya filamu,  Joyce Fissoo ili kuelezea juu ya sekeseke hilo, ziligonga mwamba hadi gazeti hili linaingia mtamboni lakini imedaiwa kuwa bodi hiyo itasimamia msimamo wake. 

No comments:

Post a Comment