Aneth Gasto akiwa hospitalini
MAMA wa mtoto, Anneth Gasto anayedaiwa kuchomwa moto na kulazimishwa
kula kinyesi na mama yake mdogo na kumsababisha mkono mmoja kukatwa
mara baada ya kufikishwa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya , Asera
Mkandara tayari amewasili mkoani hapa jana (juzi) usiku.
Akizungumza kwa uchungu huku akitokwa na machozi katika hospitali
hiyo mjini Mbeya , mama huyo alisema kuwa hajui nini kimemtokea mtoto
wake hadi kufikia kukatwa mkono na kwamba anamshukuru Mungu kwa kumkuta
mtoto wake akiwa hai.
Alisema kuwa alipata taarifa kutoka kwa ndugu zake kwamba anahitajika
Mbeya mara moja mtoto amepatwa na matatizo makubwa na kusikia taarifa za
mtoto wake huyo kupitia vyombo vya habari.
Mama huyo alisema kuwa huyo ni mtoto wake wa Pili ambapo wa kwanza
anaishi na bibi yake na kwamba huyo Anneth alichukuliwa na kaka yake
ambaye alimuhitaji kwa lengo la kutaka kumlea.
Alipohojiwa kama baba wa mtoto huyo yupo alijibu kuwa baba wa mtoto huyo
waliachana naye mwaka 2008 “ndipo kaka yangu alipo muhitaji mtoto
wangu aje aishi naye huku Mbeya.”alisema na kuongeza:
“Nasikia uchungu sana kwa yaliyomkuta mtoto wangu kwani Mungu ndiye
anayejua, nawashukuru madaktari kwa kuokoa maisha yake na wale wote
waliohusika katika kumuokoa na kumleta mtoto hapa hospitali sina cha
kuwalipa Mungu ndiye atakaye walipa”alisema.
Mwanamke anayedaiwa kumfanyia unyama mtoto huyo alifikishwa katika
mahakama ya Wilaya ya Mbeya juzi kujibu shtaka linalomkabili, ambapo
mshtakiwa alikana shitaka hilo na alirudishwa mahabusu hadi Novemba
22, Mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.
Mwendesha mashtaka wa Serikali, Achiles Mulisa aliiambia Mahakama kuwa
Mtuhumiwa Wilvina Mkandala (24) alitenda kosa la kusababisha majeraha
akiwa na nia ovu ambayo imemsababishia ulemavu mtoto Anneth.
chanzo: mwananchi