MAHAKAMA ya
Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza, imemhukumu kwenda jela miezi mitano Katibu
wa Chadema Wilaya ya Ilemela, John Anajus huku ikiwatoza faini ya
Sh620,000 viongozi wengine akiwamo Mkurugenzi wa Oganaizesheni wa
Chadema Taifa, Benson Kigaila na madiwani wawili.
Hukumu hiyo
ilitolewa kufuatia watuhumiwa hao kudharau amri ya mahakama iliyotolewa
na Hakimu Mkazi Mfawidhi mkoani Mwanza, Angelo Rumisha kufuatia kesi
namba 69/2012.
Kesi
hiyo ilifunguliwa na Henry Matata aliyekuwa Diwani wa Chadema Kata ya
Kitangiri, baada ya kuvuliwa uanachana kwa kukiuka katiba ya chama,
ambaye aliweka pinganizi la kuteua mgombea umeya Wilaya ya Ilemela.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Rumisha
alisema mahakama haiwezi kudharauliwa pale inapotoa maagizo yake, hivyo
imewatia hatiani kwa kukaidi agizo lake ili iwe fundishi kwao na
wengine.
Hakimu
Rumisha aliwatoza faini ya Sh155,000 kila mmoja watuhumiwa, huku John
Anajus ambaye hakuwapo mahakamani akihukumiwa kifungo cha miezi mitano
jela atakapopatikana.
Watuhumiwa
ambao walilipa faini ni Kigaila, Katibu wa Mwenezi wa Chadema Wilaya ya
Ilemela, Kalod Majura, Diwani wa Kata ya Kirumba, Dan Kahungu na
aliyekuwa Meya wa Mwanza ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Tendaji ya chama
hicho, Josephat Manyerere.
Katika kesi
hiyo, Matata anayetetewa na Wakili Salum Magongo, aliweka pingamizi
mahakamani baada ya Kamati Tendaji ya Chadema kutangaza kumvua uanachama
kinyume cha taratibu na kudai kwamba, viongozi hao kwa pamoja
walishiriki kuvunja sheria kwa kumtangaza kumfukuza udiwani.
Hivyo, kudaiwa kupuuza amri halali ya mahakama iliyotolewa Septemba 15, mwaka huu.
Hata hivyo, Diwani huyo alivuliwa
uanachama na Kamati Kuu ya Chadema Septemba 9, mwaka huu kutokana na
madai ya kuvunja katiba ya chama hicho, mpaka kuchaguliwa kuwa Meya wa
Manispaa ya Ilemela alikuwa amefungua kesi mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa
wa Mwanza akiomba mahakama imrejeshee uanachama wake.
Hata hivyo,
katika hatua ya kuwanusuru madiwani hao kufungwa, wananchama wa chama
hicho ambao walikuwa wamefurika mahakamani hapo walichanga Sh250,000 na
Sh370,000 zingine zililipwa na Mbunge wa Ilemela,Samson Kiwia.
Chanzo - Mwananchi