MAKAMU
Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula amekunjua makucha na kusema
walioshinda katika chaguzi za chama hicho kwa rushwa wajiandae
kung’olewa ndani ya miezi sita ijayo. Mangula
alisema hayo jana katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam
mbele ya Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete katika sherehe
zilizoandaliwa na mkoa wa Dar es Salaam kuwapongeza kwa kuchaguliwa
kwao.
Kauli hiyo
nzito ya Mang’ula imekuja siku chache tangu kumalizika kwa chaguzi za
ndani za CCM ambazo zililalamikiwa na baadhi ya makada kwamba baadhi ya
walioshinda walitumia kiasi kikubwa cha fedha kununua kura.
Miongoni mwa
chaguzi zilizolalamikiwa ni katika baadhi ya wilaya na mikoa, lakini
zaidi zile za jumuiya za chama hicho; Umoja wa Wanawake (UWT), Umoja wa
Vijana (UVCCM) na Jumuiya ya Wazazi.
Itakumbukwa
kuwa ni kutokana na hali hiyo, Rais alisema waziwazi wakati akifunga
mikutano ya UWTna Wazazi na wakati wa kufungua ule wa UVCCM kwamba
vitendo hivyo vitakipeleka chama hicho kubaya ikiwa havitakomeshwa.
Habari
kutoka ndani ya CCM zinasema tayari chama hicho kimepokea malalamiko
mengi kuhusu kukiukwa kwa taratibu za uchaguzi ndani ya chama hicho
nyingi zikihusu rushwa lakini zaidi zinaztokana na chaguzi za jumuiya za
chama hicho.
Mkakati wa Mangula
Jana Mangula alisema atatumia nafasi
yake ya Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu na Maadili aliyopewa kuwang’oa
waliopata uongozi kwa rushwa na kwamba “hatamwogopa kigogo yoyote wala
hatamwonea mtu”.
Alisema
watafanya uchunguzi wa kina kwa waliohusika na rushwa katika uchaguzi
huo bila kuihusisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
“Hakuna mla
rushwa atakayepona katika hili kwa sababu tunataka kurudisha heshima ya
chama chetu ambayo imepotea kwa sababu ya walarushwa wachache,” alisema
Mangula.
Aliongeza
kuwa katika uchanguzi huo, hata waliokuwa wakisaidia kufanikisha rushwa
hizo katika uchaguzi huo watachukuliwa hatua watakazostahili.
Mangula alisema anataka kuwaonyesha Watanzania kwamba hata wakulima wa nyanya wanaweza kufanya kazi ya kupambana na rushwa.
“Namshukuru
Kikwete kwa imani yake aliyoionyesha kwangu hadi akaniteua kugombea
nafasi hii, sitamwangusha, nitamwonyesha kuwa hata wakulima wa nyanya
wanaweza,” alisema Mangula huku akishangiliwa na halaiki ya wana CCM
waliofurika kwenye viwanja hivyo.
Kadhalika Mangula aliwaponda baadhi ya wana wanaCCM ambao wamekuwa wakinunuliwa kwa kupewa rushwa.
“Jamani
wanaCCM wenzangu acheni kununuliwa kwa kupewa sambusa na vigogo hawa wa
rushwa ni aibu, fuateni maadili ya chama chetu,” alisema Mangula.
Alisema
kuwa anataka chama hicho kirudishe heshima yake kwa kusimamia maadili
ya chama hicho ambayo yameanza kupotezwa na watu wachache.
Kinana na rushwa
Naye Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdurahaman Kinana aliesema chama hicho kina wanachama wachache ambao ni vigogo wa rushwa.
Alisema kati ya wanachama 5,000 wa CCM waliopo, asilimia 0.01 ndiyo wanaojihusisha na rushwa.
“Hawa
tutabanana nao kwa sababu ni wachache sana kuweza kukiharibu chama
chetu, tunaomba ushirikiano wa wanachama,” alisema Kinana.
Alisema ni lazima vigogo wa rushwa washughulikiwe kwa sababu ndiyo wanaowafanya wananchi wapoteze imani ya chama tawala.
“Hatuwezi kuongoza nchi wakati watu wana mashaka na sisi, hii si kazi ya viongozi pekee yao bali wana CCM wote,” alisema Kinana.
Alisema kuwa kukithiri kwa rushwa kutasababisha kupatikana kwa watu wasiokuwa makini na kukipotezea chama mwelekeo.
Rais Kikwete
Kwa upande wake Rais Kikwete aliwataka
viongozi wa CCM waliochaguliwa kufanya kazi kwa bidii ili kurudisha
imani ya wananchi ambayo ilianza kupotea.
“Viongozi mliochaguliwa jisikieni kuwa mna deni kubwa la Watanzania ambao wengi wao wameanza kukata tamaa,” alisema Kikwete.
Aliwataka
kujibu mapigo ya viongozi wa vyama vya upinzani kwa sababu wakikaa kimya
wananchi watafahamu kwamba ni kweli wanayoyazungumza.
Chanzo - Mwananchi