MKUU WA MKOA Dodoma, Dk. Rehema Nchimbi amewataka wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu walioko katika mkoa huo kujihoji
nafsi zao na kucheki matendo yao kama kweli ni ya kumpendeza Mungu kwa
vile ndiyo yanachangia wao kutotambua umuhimu wa nafasi walizonazo.
Dk. Nchimbi ametoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati akihutubia maelfu ya wanavyuo waliohudhuria Jumuiko la Wanavyuo
wa Dodoma (Dodoma Campus Night) lililoambatana na mkesha wa kusifu na
kuabudu uliofanyika kwenye ukumbi wa Chimwaga mjini Dodoma.
Jumuiko hilo lilihudhuriwa na
wanafunzi zaidi ya 3,500 wa dini mbalimbali kutoka vyuo vikuu vya Dodoma
(UDOM), St. John’s, Vyuo vya Mipango, Madini, Mirembe, Hombolo, Chuo
cha Elimu ya Biashara (CBE) na vyuo vya ualimu vya Mitumba na Capital.
Dk. Nchimbi alisema wanavyuo
wengi ambao walifaulu kidato cha sita kwa alama za juu (first class)
huwa wanaporomoka kimasomo wanapoingia kwenye vyuo vya elimu ya juu kwa
sababu hawajiweki sawa kwenye mahusiano yao na Mungu aliyewaumba.
“Wanaharibikiwa kwa sababu hawajiweki sawa na Mungu… hawakai pale ambapo
Mungu anataka wawe (their right position),” alisema.
“Tunzeni nafasi zenu ambazo
Mungu amewapatia… uwingi wenu huu katika usiku wa leo hauna maana kama
hatutakuwa na uhusiano mwema na Mungu kwani hata shetani ana watu wake
na huwa anawapatia mahitaji yote… kila mmoja wenu aanze upya na Mungu”,
alisema.
“Tumfikirie Mungu, tuangalie
mahusiano yetu na Mungu wetu yakoje na tumuombe atusaidie katika yote
tuyatendayo, naye atatujibu kwa sababu Mungu huwa hawekezi kwa hasara
bali huwekeza kwa faida,” alisema huku akishangiliwa na wanafunzi
waliokuwa wamefurika kwenye ukumbi huo.
Alisema idadi kubwa ya wanavyuo
wakishapata fedha za mkopo hutumbua maisha kwenye vilabu vya muziki
ambavyo ni maarufu mjini humo kama vile Club 84, Club La Aziz na Maisha
Club na hawarudi vyuoni hadi fedha yote imekwisha.
“Mungu alipofanya uumbaji
alisema kila alichokifanya ni chema sana. Sasa kama wewe ni kiumbe chema
wa Mungu iweje uende kwenye hizo club kuponda maisha, iweje unywe
pombe, iweje ufanye uzinzi na uasherati badala ya kukaa chuoni ukasoma,
iweje ugome kufanya mtihani hadi upate ‘kibuti’?, alihoji huku
akishangiliwa na wanavyuo hao.
Alisema yeye kama mzazi
analazimika kuyasema hayo kwa sababu anatambua kuwa watoto wa leo
wamezungukwa na mitego mingi. “Hatutaki shetani awachezee, ndiyo maana
tunawaonya,” alisisitiza.
Alisema katika kundi kubwa kama
hilo wamo viongozi wa kesho na kwamba wasipojihadhari na kuweka
mahusiano yao sawa na Mungu kuanzia sasa, watajikuta wanafanana na
baadhi ya viongozi nchini ambao wamekabidhiwa dhamana lakini
wanakengeuka na kufanya kinyume na matarajio ya wengi.
Akitoa mfano alisema: “Nchi hii
wako wasomi wengi lakini wamekaa kiwiziwizi tu, fedha za barabara
zikitolewa haziendi kufanya kazi iliyopangwa, wakurugenzi wakipewa fedha
za kujenga shule, mabweni au nyumba za walimu, unakuta zinakamilika
lakini ziko chini ya kiwango, madaktari nao wanaiba dawa za hospitali
kwa kutumia magari ya kubebea wagonjwa.”
“Kama viongozi hawa wangesimama
kwenye nafasi zao (right position) haya mambo yangetoka wapi? Mambo ya
mikataba mibovu yangetoka wapi? Mnadhani nchi hii ingekuwa maskini?
Haiwezekani!” alisisitiza huku akishangiliwa na wanavyuo hao.
Aliwasihi wanavyuo wote watambue
nafasi zao na wazitunze nafasi hizo ili wasimkosee Mungu. “Tunzeni
nafasi zenu mlizopewa na Mungu na wakati wote jitahidini kusikiliza
sauti yake, muone jinsi atakavyowashindia”, alisema.
Mapema, akimkaribisha Mkuu wa
Mkoa kuzungumza na wanafunzi hao, Mchungaji Gerald ole Nguyaine wa
Kanisa la ICC –TAG Dodoma alisema wanafunzi walio katika vyuo hivyo ni
wababa na wamama wa kesho hivyo hawana budi kumtanguliza Mungu katika
yote wayafanyayo.
Naye Mchungaji Gavin Walker
kutoka Kanisa la Calvary Christian Fellowship lililoko Columbus, Ohio,
Marekani ambaye alikuwa mnenaji mkuu katika mkesha huo, aliwasihi
wanavyuo kutambua makusudi ya Mungu ambayo ameyaweka juu yao. “Mungu
amekuumba wewe kwa kusudi maalum hivyo ni lazima ujue hilo kusudi”,
alisema.
Alisema kwa kutotambua kusudi la
Mungu katika maisha yao, wako watu ambao wamejikuta wakitaka kufanana
na wengine bila kujua ni kwa nini watu hao wamekuwa hivyo. “Wanatamani
nafasi za wengine kwa sababu tu wao ni maarufu, ni waigizaji, ni wacheza
sinema ama wasanii… hapana! Kila mmoja anatakiwa kujua kusudi ka Mungu
katika maisha yake,” alisisitiza.
Alisema duniani kuna wakazi
zaidi ya bilioni saba lakini wengi kati ya hao wanaishi maisha
yasiyotimilika kwa sababu hawamjui Mungu. “Hakuna kitu ambacho Mungu
hawezi kukifanya maishani mwetu, tunachotakiwa ni kumuomba tu! Kama ni
masomo soma kwa bidii huku ukimtumaini Mungu, nawe utashinda sababu
Mungu yuko upande wako,” alisisitiza.
Aliwaasa wawe wavumilivu wawapo
vyuoni. “Katika maisha ya chuo jifunze kuwa na saburi. Ukijenga saburi
sasa hivi tangu uko chuoni, itakusaidia kuvumilia mengi katika maisha ya
mbele baada ya kuhitimu Chuo Kikuu au chuo chochote unachosoma sasa,”
alisisitiza.