November 19, 2012

Philip Mangula ahaidi katika miezi sita yake ya utendaji wake wale wote waliochaguliwa kwa rushwa wajijue wamepoteza hizo nafasi zao.




MAKAMU Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula amekunjua makucha na kusema walioshinda katika chaguzi za chama hicho kwa rushwa wajiandae kung’olewa ndani ya miezi sita ijayo. Mangula alisema hayo jana katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam mbele ya Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete katika sherehe zilizoandaliwa na mkoa wa Dar es Salaam kuwapongeza kwa kuchaguliwa kwao.
“Wote walioleta malalamiko yanayohusu rushwa katika uchaguzi watulie, tunayashughulikia, kama kuna mtu alipita kwa rushwa afahamu kuwa amepoteza,” alisema Mangula ambaye anasema kabla ya kuteuliwa alikuwa anajishughulisha na kilimo cha nyanya na maparachichi.
Kauli hiyo nzito ya Mang’ula imekuja siku chache tangu kumalizika kwa chaguzi za ndani za CCM ambazo zililalamikiwa na baadhi ya makada kwamba baadhi ya walioshinda walitumia kiasi kikubwa cha fedha kununua kura.
Miongoni mwa chaguzi zilizolalamikiwa ni katika baadhi ya wilaya na mikoa, lakini zaidi zile za jumuiya za chama hicho; Umoja wa Wanawake (UWT), Umoja wa Vijana (UVCCM) na Jumuiya ya Wazazi.
Itakumbukwa kuwa ni kutokana na hali hiyo, Rais alisema waziwazi wakati akifunga mikutano ya UWTna Wazazi na wakati wa kufungua ule wa UVCCM kwamba vitendo hivyo vitakipeleka chama hicho kubaya ikiwa havitakomeshwa.
Habari kutoka ndani ya CCM zinasema tayari chama hicho kimepokea malalamiko mengi kuhusu kukiukwa kwa taratibu za uchaguzi ndani ya chama hicho nyingi zikihusu rushwa lakini zaidi zinaztokana na chaguzi za jumuiya za chama hicho.

Mkakati wa Mangula
Jana Mangula alisema atatumia nafasi yake ya Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu na Maadili aliyopewa kuwang’oa waliopata uongozi kwa rushwa na kwamba “hatamwogopa kigogo yoyote wala hatamwonea mtu”.
Alisema watafanya uchunguzi wa kina kwa waliohusika na rushwa katika uchaguzi huo bila kuihusisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
“Hakuna mla rushwa atakayepona katika hili kwa sababu tunataka kurudisha heshima ya chama chetu ambayo imepotea kwa sababu ya walarushwa wachache,” alisema Mangula.
Aliongeza kuwa katika uchanguzi huo, hata waliokuwa wakisaidia kufanikisha rushwa hizo katika uchaguzi huo watachukuliwa hatua watakazostahili.
Mangula alisema anataka kuwaonyesha Watanzania kwamba hata wakulima wa nyanya wanaweza kufanya kazi ya kupambana na rushwa.
“Namshukuru Kikwete kwa imani yake aliyoionyesha kwangu hadi akaniteua kugombea nafasi hii,  sitamwangusha, nitamwonyesha kuwa hata wakulima wa nyanya wanaweza,” alisema Mangula huku akishangiliwa na halaiki ya wana CCM waliofurika kwenye viwanja hivyo.
Kadhalika Mangula aliwaponda baadhi ya wana wanaCCM ambao wamekuwa wakinunuliwa kwa kupewa rushwa.
“Jamani wanaCCM wenzangu acheni kununuliwa kwa kupewa sambusa na vigogo hawa wa rushwa ni aibu, fuateni maadili ya chama chetu,” alisema Mangula.
Alisema kuwa anataka chama hicho kirudishe heshima yake kwa kusimamia maadili ya chama hicho ambayo yameanza kupotezwa na watu wachache.

Kinana na rushwa
Naye Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdurahaman Kinana aliesema chama hicho kina wanachama wachache ambao ni vigogo wa rushwa.
Alisema kati ya wanachama 5,000 wa CCM waliopo, asilimia 0.01 ndiyo wanaojihusisha na rushwa.
“Hawa tutabanana nao kwa sababu ni wachache sana kuweza kukiharibu chama chetu, tunaomba ushirikiano wa wanachama,” alisema Kinana.
Alisema ni lazima vigogo wa rushwa washughulikiwe kwa sababu ndiyo wanaowafanya wananchi wapoteze imani ya chama tawala.
“Hatuwezi kuongoza nchi wakati watu wana mashaka na sisi, hii si kazi ya viongozi pekee yao bali wana CCM wote,” alisema Kinana.
Alisema kuwa kukithiri kwa rushwa kutasababisha kupatikana kwa watu wasiokuwa makini na kukipotezea chama mwelekeo.

Rais Kikwete
Kwa upande wake Rais Kikwete aliwataka viongozi wa CCM waliochaguliwa kufanya kazi kwa bidii ili kurudisha imani ya wananchi ambayo ilianza kupotea.
“Viongozi mliochaguliwa jisikieni kuwa mna deni kubwa la Watanzania ambao wengi wao wameanza kukata tamaa,” alisema Kikwete.
Aliwataka kujibu mapigo ya viongozi wa vyama vya upinzani kwa sababu wakikaa kimya wananchi watafahamu kwamba ni kweli wanayoyazungumza.
Chanzo - Mwananchi