Blogger Widgets

May 29, 2013

sisi tutashiriki, wewe je?? Huu Ni Ujumbe wa Issa Michuzi Juu ya Show ya Lady Jay Dee na Kuamua Kufunguka Live wa Mabaya Anayofanyiwa Lady Jay Dee


Kuna mambo kusimamiwa kwake kidete ni kukaa chini, mengine ni kulala na mengine ni kusimama wima. Kukiwa na jambo au hali haulidhiki nayo, machaguo yako mengi kuonyesha hisia na hata msimamo wako. Yote haya lazima yafanyike maadamu tu ujumbe ufike kwa ufasaha mahala husika wakati hatua sahihi zikiendelea na utekelezwaji. Haiwezekani kwenye nchi yenye tatizo la ajira linaloongezeka kila uchao vijana wenye vipaji wafe na njaa kisa tu ugomvi na madalali wa sanaa! 
Wasanii wanapaswa kufa na njaa pale tu kama kazi zao hazikubaliki na hadhira na hivyo hazinunuliki. Lakini suala la kufichwa na kufunikwa kwa jitahada za nguvu ya uwezo wa kifedha, mali na mtandao mpana ni la kupingwa kwa nguvu zote na hadhira. Lazima hadhira iwe ndiyo hakimu pekee wa kazi, maslahi na mafanikio ya wasanii. Haiwezekani hadhira ionekane ni ya muhimu tu katika kauli mbiu za kuteka masoko kibiashara lakini linapokuja suala la mahitaji, hadhira ichaguliwe na fanani nini inastahili kusikia, kuona, au kula. Hili kamwe haliwezi kuwa chaguo langu wala la hadhira au Watu. 
Ni chaguo la fanani na la stahili kusikilizwa, kuonwa au kuliwa na huyo huyo fanani na mafanani wenzake. Dhihaka inakuwa kubwa zaidi pale jambazi linapoongoza jitihada ya kutokomeza kazi za vibaka! Kweli mwenye nacho hujitwalia zaidi na sheria ni kipofu kwa mwenye nacho. Pamoja na yote haya, umma unayo silaha nzito na mahsusi yenye uwezo wa kuwaangamiza majambazi na kuwatokomeza vibaka. Silaha yetu ni umoja katika kupinga ufedhuri wa mafanani uchwara na dhihaka ya majambazi. Anayejitenga na umoja huu, anajindalia upweke msibani zamu yake ikifika. 
Ni masikitiko kwamba wanaodhurumiwa na kuibiwa wameanguka katika tego la kale la majambazi na wadhurumaji. Wametegwa wajitenge na umoja na wao kwa kujua ama kwa kutokujua wakategeka! Wamekubali kuutumikia mkate wa siku wa kafiri wasijue kwamba kesho safari ya dhuluma yaendelea! Na hawa watadumu katika safari ya kudhulumiwa milele na hawachomoki ng’o! Tunaochukizwa na yote yaliyosimuliwa hapo juu, tuungane na waliokwisha jitambua katika kujinasua na ufedhuri wa madalali uchwara wa sanaa. 
Tuwasaidie kupaza sauti za umoja katika kuwashambulia majambazi. Tuwaonyeshe mafanani uchwara na majambazi kwamba nguvu haziko kwao bali kwetu (hadhira). Tulidhirishe kwamba sisi ndiyo tunapaswa kuchagua tukipendacho maana twalipia muda, huduma na bidhaa. 
Tukatae kuchagulia nini kisikilizwe na masikio yetu, macho yetu yaone nini au vinywa vile nini na kisha watupigie kauli mbiu za “Chaguo la Watu” Ijumaa ya Tarehe 31 mwezi huu, tuliowengi hatuendi na kipaumbele cha kucheza disco, kuangalia wacheza disco au kusikiliza music live bali tunakwenda kusema hapana: “Unyonyaji haukubaliki na Kufanyiwa machaguo hakukubaliki”. Tutafanya hivyo kwa sauti kubwa na ya umoja. Tunakwenda kuthibitisha kuwa ni Sisi ndiyo hadhira na siyo wao.
From:Issa Michuzi