Blogger Widgets

December 30, 2013

soma na Tazama Jinsi Mlolongo Uliosababisha Jack Cliff Kukamatwa na Madawa ya Kulevya Huko China

 
Jack akiwa chini ya ulinzi.
Stori: Stori: waandishi Wetu
MADAI ya kukamatwa kwa tuhuma za kumeza madawa ya kulevya aina ya Heroin nchini China kwa msanii, Video Queen na mwanamitindo maarufu Bongo, Jacqueline Patrick, kumeibua maswali ya kila aina,  mengi yamesemwa, uvumi umeenea, lakini Ijumaa Wikienda linadondosha hatua kwa hatua.

Baada ya kuinyaka taarifa hiyo ya aibu kwa staa huyo na taifa kwa jumla, kwa uchungu mkubwa timu yetu imara ilijipanga na kuingia mtaa kwa mtaa, nyumba kwa nyumba, mtu kwa mtu kuchimbua, kudadavua na kufukunyua kwa undani zaidi juu ya tuhuma hizo. Aya zinazofuata zitakupa mwanga.
ALIVYONASWA HATUA KWA HATUA
Wikienda lilichorewa mchoro kwamba, Jack alikamatwa Desemba 19, mwaka huu katika Uwanja wa Ndege wa Macau nchini humo akitokea jijini Bangkok nchini Thailand kuelekea Guangzhou, Mji Mkuu wa Jimbo la Guangdong Kusini mwa China.

NINI KILISABABISHA?
Inadaiwa kuwa miongoni mwa mambo yaliyochangia kunaswa kwake ni uso wa uchovu, kuanza kuwa na hali mbaya ya mwili, kushindwa kujibu maswali vizuri na hati yake ya kusafiria (passport) yake kuonesha kugongwa mihuri ya kuingia nchini humo kila mara.

Habari zinasema ndipo maafisa wa uwanja huo walipomweka pembeni na baadaye kumpeleka kwenye chombo cha kukagua kwa undani mwili wa binadamu, walipojiridhisha ana ‘mzigo’ wakampa polisi mwanamke (WP) kwa ajili ya kwenda kusimamia utoaji wa kete hizo chooni kwa njia ya haja kubwa.
AVALISHWA MASKI, AWEKWA MBELE YA MAPAPARAZI
Baada ya kutoka chooni, ikafuata hatua nyingine. Jack aliwekwa mbele ya mapaparazi akiwa amevalishwa maski nyeusi usoni ili asionekane sura kisha akapigwa picha za kumwaga.
Sheria za Macau, mtuhumiwa huvalishwa maski usoni ili watu wasiione sura yake. Kete alizozitoa ziliwekwa juu ya meza, pia simu zake mbili, Iphone na Samsung nyeupe zilikuwa pembeni. Baadhi ya watu Bongo walizitambua simu hizo kwamba ni zake.

AINA YA MADAWA
Jack ambaye ni Miss Ilala Namba 3, 2005, alikamatwa na madawa aina ya Heroin yenye uzito wa kilo 1.1 yakiwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni 223 kwa kuhifadhiwa ndani ya kete 57.

ATANYONGWA?
Kwa sheria za Beijing, China mtu akithibitika kubeba unga hukumu yake ni kunyongwa tu lakini waandishi wetu walipozungumza na wataalam mbalimbali wa sheria za kimataifa ili kujua ni adhabu gani inaweza kutolewa kwa mrembo huyo endapo atakutwa na hatia, walisema Beijing si Macau, ni vigumu kula kitanzi lakini kwenda jela miaka mitatu, minne au nane inaweza ikamhusu. Majimbo mengi ya China yanaongozwa kwa sheria zake badala ya sheria mama moja kwa nchi nzima.

Hata hivyo, sheria za eneo alilokamatiwa zinasema kuwa uwezekano wa ndugu, jamaa na marafiki kumuona kwa sasa haupo mpaka Machi, 2014 uchunguzi utakapokuwa umekamilika.
WATU WA KARIBU WALIVYOPOKEA TAARIFA
Awali, baadhi ya watu wa karibu na modo huyo waligoma kuweka bayana kuhusu yaliyompata Jack huko ughaibuni wakidai si wasemaje wake na kuwataka mapaparazi kwenda kuchimba kwenye Ubalozi wa China nchini Tanzania.

Kwa sharti la kutotajwa jina mahali popote kwenye ukurasa huu, mmoja wa marafiki wa karibu wa Jack aliyeko China kwa masomo, alisema amethibitisha ukweli kupitia balozi ndogo ya Tanzania nchini humo.
“Nilishituka sana niliposikia habari hizo, ikabidi nijiridhishe kwa kwenda kwenye ubalozi mdogo wa Tanzania nchini hapa na kupewa maelezo kamili juu ya sakata hilo.

“Nikaulizia uwezekano wa kuonana na Jack, nikaambiwa ni ngumu kutokana na utata mkubwa juu ya ishu yenyewe,” alisema rafiki huyo na kuongeza:
“Hata jana (Jumatano ya wiki iliyopita) gazeti moja liitwalo Daily China la huku lilitoa habari hiyo ndipo nikathibitisha baada ya kuona sura gazetini. Kweli ni Jack Patrick, najisikia uchungu na huruma juu yake, inauma lakini hatuna jinsi,” alisema rafiki huyo.

NYUMBANI KWAKE KAMA MSIBA
Kazi ni kazi tu. Timu yetu ikiwa na kiu, hamu na shauku kubwa ya kuujua ukweli, ‘ilisaga lami’ mguu kwa mguu hadi kwenye nyumba aliyokuwa anaishi Jack iliyopo Mikocheni B jijini Dar ili kuona hali ikoje na kujiridhisha zaidi ambapo iliashiria kila dalili ya kuwepo kwa habari mbaya.

Ukimya, utulivu na hali ya kupoa viliitawala nyumba hiyo baada ya waandishi wetu kuwasili na kukuta hakuna chochote zaidi ya milio ya ndege iliyokuwa ikisikika.
Mmoja wa waandishi wetu alipanda ukuta na kuchungulia ndani ambapo hakuona binadamu isipokuwa gari lake lile Benz jeusi likionekana liliegeshwa siku nyingi.

MAJIRANI HAWA HAPA
Roho za kutoridhika ziliwasukuma mapaparazi wetu kuwatafuta majirani wa msanii huyo ili kusikia walau chochote kipya kuhusiana na taarifa za Jack kunaswa na unga.
“Mh! Hata sisi hatujui maana hatujamuona siku mbili hizi, lakini kama ni kusikia hata sisi tumesikia juu ya uvumi huo, lakini hatuna uhakika,” alisema mama mmoja (jina linavunda kwenye droo zetu).

NANI YUKO NYUMA YA JACK?
Watu wengi (tukiwemo sisi) wana hamu kubwa ya kujua ni nani hasa anahusika na mzigo ambao msanii huyo anatuhumiwa kukamatwa nao. Katika pitapita ya waandishi wetu kupeleleza kwa undani suala hili, lilibahatika kuzungumza na baadhi ya watu ambao walihoji na kutaka kujua ni kigogo yupi yuko nyuma ya ishu nzima.

“Lazima kutakuwa na mtu nyuma yake, si bure nyie fuatilieni sana,” alisema mdau mmoja ambaye hakupenda jina lake litajwe mahali popote.
Aliongeza kuwa, mtu anayekutwa na kete za unga tumboni maana yake katumwa (punda) na bosi wake, kwa hiyo suala kubwa kwa sasa ni kumsaka bosi huyo ili afikishwe kwenye vyombo vya sheria.

UWANJA WA NDEGE DAR MATUMBO JOTO
Hakuna ubishi kwamba hali ni mbaya kwa wafanyakazi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Kambarage jijini Dar, kwa madai kuwa piga, ua, galagaza mzigo huo, Jack alikatiza nao pale.
“Jack alitokea Dar kwenda Thailand kupitia Nairobi, lazima mzigo alitoka nao Bongo, tena jijini Dar. Sasa pale eapoti alipitaje? Serikali iwachunguze wafanyakazi wa pale,” alisema nguli mmoja wa filamu za Bongo (jina lake lipo).

NI ZAIDI YA MASOGANGE
Hii imekaa vibaya! Wataalam mbalimbali wa masuala ya kisheria walizungumza na gazeti hili juzi na kusema kuwa sakata la Jack ni kubwa zaidi ya lile la Agnes Gerald ‘Masongange’ na nduguye, Melisa Edward  waliokamatwa nchini Afrika Kusini Julai 5, mwaka huu.

NI AIBU KWA TAIFA
Wakizungumza na Wikienda kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi walisema tukio la Jack limezidi kuchagiza aibu kubwa kwa taifa katika medani za kimataifa kufuatia matukio mengi ya Watanzania kukamatwa na madawa ya kulevya nje ya nchi.

MSIKIE NZOWA
Akizungumzia suala hilo, Kamanda wa Polisi Kitengo cha Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya Tanzania, Godfrey Nzowa alisema taarifa hizo zilimfikia kutoka kwa watu mbalimbali wakiwemo waandishi wa habari, hivyo anaendelea kufuatilia suala hilo kwa ukaribu zaidi ili kupata taarifa sahihi.

Aidha, Kamanda Nzowa alisema kuna wakati aliyekuwa mume wa mwanamitindo huyo, Abdulatif Fundikira aliwahi kukamatwa na madawa za kulevya nchini na kuachiwa kwa dhamana, ina maana kesi bado ipo mahakamani.