Golikipa
hodari nchini, Juma Kaseja jana(Novemba 08,2013) amesaini Mkataba wa miaka
miwili na klabu ya Yanga SC kwa Shilingi Milioni 40.
Kaseja amesainshwa na vigogo wa Usajili wa Yanga, Abdallah Ahmed Bin Kleb na Seif
Ahmed ‘Magari’ mbele ya Meneja wake, Abdulfatah Salim Saleh Ilala mjini Dar es
Salaam.
Kaseja sasa anakwenda kuungana na makipa wawili aliowahi kufanya nao kazi Simba
SC, Ally Mustafa ‘Barthez’ na Deo Munishi ‘Dida’.
Hii inakuwa
mara ya pili Kaseja kusajiliwa Yanga, baada ya awali kusajiliwa mwaka 2009
akitokea Simba SC ambako baada ya msimu mmoja wa Mkataba wake kumalizika
akaachwa na kurejea Msimbazi.
Kaseja aliachwa Simba SC mwishoni mwa msimu kwa madai kiwango chake kimeshuka
na amelazimika kuukosa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Bara, ingawa sasa
baada ya kumwaga wino Yanga anarudi kazini Januari.
Kikubwa kilichoisukuma Yanga SC kumsajili kipa huyo ni uzoefu wake katika
michezo ya kimataifa na inataka inufaike naye katika Ligi ya Mabingwa Afrika
mwakani.