Mojawapo ya ofisi za Kampuni ya Kanumba The Great Films illiyopo Sinza Mori.
MIPANGO
endelevu inapaswa kufuatwa na kila mwanadamu, katika familia zetu za
Kiafrika mara nyingi tunaanguka katika suala la mipango mikakati ya muda
mrefu. Mwanadamu akifariki, mara nyingi wanaoachwa kuendeleza kazi za
marehemu wanaishia kusuasua na kutofikia malengo.
Yapata
mwaka mmoja tangu, aliyekuwa legend wa simema za Kibongo, Steven
Kanumba ‘The Great’ afariki dunia na kuiacha Kampuni yake ya Kanumba The
Great Film ikiendeleza shughuli zake za kuzalisha filamu kama kawaida.
Kampuni aliyoiacha pale
Sinza-Mori, jijini Dar ilibaki chini ya mikono ya wafanyakazi wake
wakiongozwa na mdogo wa marehemu, Seth Bosco, mpiga picha za video,
Zakayo Magulu pamoja na Mayasa Mrisho ‘Maya’ ambaye alikuwa akifanya
kazi kama msimamizi wa ‘location’ (location manager) na masuala ya
makeup.
Kadiri siku zilivyozidi
kusonga, umoja kati yao ulianza kupungua. Kila mmoja anaonekana
kuhangaika kivyake licha ya kwamba kampuni bado ipo. Mikakati ya jumla
ikawa haijadiliwi, kila mmoja akawa anaangalia namna ya kujikwamua
kivyake.
Mara kadhaa nimekuwa
nikizungumza na baadhi ya wasanii waliokuwa tegemezi katika kampuni
hiyo, wamekuwa wakiniambia wapo bize kufanya kazi zao binafsi nje ya
Kanumba The Great Film. Hiyo inaonesha dalili kwamba kazi za umoja
zimeanza kulegalega.
Marehemu Steven Kanumba akiwa na tuzo za filamu enzi za uhai wake.
Miongoni
mwa bidhaa zilizokuwepo katika ofisi hiyo ni pamoja na DVD za marehemu
alizokuwa akiziuza lakini baada ya kifo chake, ofisi hiyo imepoteza
mvuto wa kibiashara na hata mpangilio kwa jumla. Hakuna mtu wa kukemea
au kuhakikisha mambo yanakwenda sawa.
Kabla Kanumba hajapatwa na
mauti, alikuwa mpiganaji. Alipambana kuhakikisha anafikia malengo yake.
Lengo lake lilikuwa ni kuhakikisha tasnia ya filamu inafika levo za
Kimataifa.
Enzi za uhai wake, Kanumba
ndiye aliyeanza kuthubutu kutoboa mianya ya kuwashirikisha wasanii wa
Nigeria. Alifanikiwa kucheza simema ya Dar 2 Lagos na filamu nyingine
kadhaa kwa kuwashirikisha wasanii mbalimbali wa nje ya Tanzania.
...Akiwa kazini enzi za uhai wake.
Kama
hiyo haitoshi, mwaka 2011 marehemu alizidi kujitanua zaidi katika soko
la Nollywood kwa kumchukua mwigizaji mkubwa nchini Nigeria, Ramsey Noah
na kufanya naye filamu ya Devil King Dom ambayo kwa kiasi kikubwa
imeleta mapinduzi makubwa katika gemu.
Kuonesha anapenda maendeleo,
Kanumba hakuishia hapo kwani mwaka huohuo alipiga hatua nyingine kubwa
katika sanaa baada ya kufanikiwa kwenda New York, Marekani na kununua
vifaa vya kisasa vya kuzalishia filamu.
Mpaka mauti yanamkuta Aprili
7, mwaka jana tayari alikuwa ameshajiwekea misingi mizuri katika sanaa
kwani alikuwa anamiliki kampuni yenye vifaa vya kisasa pamoja na kutoa
ajira ya wafanyakazi wasiopungua kumi.
Marehemu alijiwekea mikataba
na Kampuni ya Steps Entertainment kuzalisha filamu 6 kwa mwaka. Hilo
alifanikiwa kwa kiasi kikubwa, tena aliweza kuigiza na filamu nyingine
za kushirikishwa mbali na zile za Steps.
Hadi kufikia Aprili 7, mwaka
huu marehemu alikuwa akitimiza mwaka mmoja kaburini. Mdogo wake, Seth
Bosco ambaye amejitoa kuendeleza kampuni hiyo, amefanikiwa kuingiza
sokoni filamu tatu tu.
...Akiwa katika pozi.
Mbaya
zaidi mbili kati ya hizo (Love and Power na Ndoa Yangu) zilisharekodiwa
na marehemu, wao wakazikamilisha kwa kuzifanyia ‘editing’. Yeye kama
yeye alifanikiwa kuingiza filamu moja sokoni ya Malaika.
Kwa mwendo huo utagundua spidi
aliyoiacha marehemu imepungua, filamu walizoingiza ni chache sana.
Kifupi wanasuasua kama si kupoteza muelekeo. Kwa mfumo aliokuwa akienda
nao marehemu, mwaka mmoja baada ya kifo hadi sasa, kampuni ilipaswa
kuzalisha filamu sita au zaidi.
Kuna kitu cha kujifunza katika mfumo ambao aliuacha marehemu. Walioachiwa kampuni wakiongozwa na Seth wanapaswa kujitazama upya.
...Akiandaa filamu ya Devil's Kingdom aliyocheza na Ramsey (kulia).
Hii
ni changamoto ngumu inayohitaji akili ya ziada kuweza kuvuka, katika
hali kama hiyo hakuhitaji masihara wala utani hata kidogo. Hapo ndipo
watu wanapotafutana uchawi. Wenye mamlaka ya kuiendesha kampuni kwa
namna moja au nyingine wanapaswa kuwa wakali kidogo ili mambo yaende.
Kujituma kwa marehemu ndiyo
kulisababisha ashinde tuzo mbalimbali za filamu zikiwemo zile za
Zanzibar Film Festival (Ziff). Ingependeza basi heshima ile aliyoiacha
marehemu ikaenziwa kwa kuvuka mipaka, ikiwezekana zaidi ya pale
alipokuwa akipapigia mahesabu yeye enzi za uhai wake.
Naamini inawezekana kama wahusika wataweka nia.
From:Audiface