ILI kuhakikisha
harudi tena kwenye matumizi ya madawa ya kulevya, jeshi la polisi
nchini, limemweka kati mwanamuziki Rehema Yusuf Chalamila ‘Ray C’.
Kamanda wa jeshi la
polisi, kitengo cha kudhibiti madawa ya kulevya nchini, Godfrey Nzowa,
amesema kuwa Ray C kila anapotembea anakuwa katikati ya askari
wanaofuatilia nyendo zake.
“Kila
anapokwenda, askari wamemzunguka. Tangu alipopata nafuu, tumekuwa
tukihakikisha havutiwi na makundi mabaya, vilevile tunataka kuona kweli
amejirekebisha,” alisema Nzowa na kuongeza:
“Ray C mwenyewe
haoni lakini kila anapotoka, askari wanamuweka katikati. Kwa kifupi
kipindi hiki tumemuweka katikati yetu, kwani hata anapokuwa nyumbani,
tunachunguza nani anaingia na anapeleka nini.”
Nzowa aliongeza
kuwa kitengo chake kimeamua kumuweka kati Ray C kwa sababu mbili, moja
ikiwa kubaini na kuwanasa wauzaji wanaomharibu mwanamuziki huyo, pili ni
kufuatilia kama msaada uliotolewa na Rais Jakaya Kikwete umefanya kazi
yake ipasavyo.
“Mheshimiwa (JK)
alitoa msaada wa matibabu kwa Ray C kwa nia njema, vilevile dada huyo
aliapa mbele yake kama hatarudia tena. Sasa ni lazima kufuatilia na
kudhibiti asije kuingia kwenye vishawishi, akakiuka kiapo na matokeo
yake alichokifanya mheshimiwa kikaonekana hakina maana,” alisema Nzowa.
Kwa upande mwingine, Nzowa alisema, hali ya Ray C inaendelea kuimarika na akaongeza: “Akili
yake imetulia, anaweza hata kutunga nyimbo tofauti na alivyokuwa. Watu
ambao anafungamana nao kwa sasa ni wazuri, siyo magenge ya wauzaji na
watumiaji wa madawa ya kulevya.”
Ray C, alisharipotiwa kuwa na hali mbaya baada ya kutopea kwenye utumiaji wa madawa ya kulevya.
Hata hivyo, JK aliamua kujitolea kunusuru maisha ya mwanamuziki huyo kwa kugharamia matibabu yake mpaka apone.
Takriban miezi
mitatu iliyopita, Ray C alitinga ikulu na kumshukuru JK kwa msaada
aliompa, vilevile akawaambia Watanzania kwamba sasa anajisikia amepona
na anaweza kufanya kazi.