Ni
orodha ndefu ya wachezaji waliohama kutoka Simba kwenda Yanga na kutoka
Yanga kwenda Simba, tangu enzi za akina Emanuel Mbele ‘Dubu’, lakini ni
wachache waliong’ara kote kote.
Athumani
Mambosasa (sasa marehemu), Zamoyoni Mogella, Method Mogella (sasa
marehemu), Hamisi Gaga (sasa marehemu), Deo Njohole, Akida Makunda,
Alphonce Modest, Monja Liseki, Shaaban Ramadhan, Eustace Bajwala, Joseph
Katuba (sasa marehemu) wote hao ni baadhi ya wachezaji waliotoka Simba
na kwenda kucheza Yanga.
Maulid
Dilunga ‘Mexico’, Ezekiel Greyson ‘Jujuman’, Justin Mtekere (wote
marehemu), Ally Yussuf ‘Tigana’, Yussuf Macho, Godwin Aswile, Ismail
Suma, Steven Nemes, Nico Bambaga, Bakari Malima, Willy Martin, Edibily
Lunyamila, Mtwa Kihwelo, Omar Hussein ‘Keegan’, Athumani China, Mohamed
Hussein ‘Mmachinga’, Mohamed Banka na Amri Kiemba wote pia ni baadhi ya
wachezaji waliotoka Yanga na kucheza Simba. Banka na Kiemba wamo kwenye
kikosi cha msimu huu (2009/10) pia.
Athumani
China akiwa Yanga, aliifunga Simba bao la mapema, dakika ya tatu,
Oktoba 9, mwaka 1991 kwenye Ligi ya Muungano, wakati watoto wa Jangwani
wakiibuka na ushindi wa 2-0. Bao la pili la Yanga lilifungwa na Abubakar
Salum ‘Sure Boy’ dakika ya 54.
China
tena aliifunga Yanga akiwa Simba, lilikuwa bao la pili katika ushindi
wa 4-1 kwa Wekundu wa Msimbazi, Julai 2, mwaka 1994. Ally Yussuf
Suleiman ‘Tigana’, pia alifunga mabao kote kote, Thomas Kipese kadhalika
naye aliwafunga Simba na baadaye Yanga.
Akida
Makunda aliihama Simba kuingia Yanga akiwa hana kumbukumbu ya kufunga
bao kwenye mechi ya watani, lakini mara baada ya kutua kwa wana Jangwani
aliingia kwenye orodha ya nyota waliofunga mabao kwenye mechi baina ya
wababe hao wa soka ya Tanzania.
Ilikuwa
Februari 21, mwaka 1998 katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania
Bara, wakati huo ikidhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia
bia yake ya Safari Lager, wakati Makunda alipofunga bao lililoelekea
kuwatoa Yanga kifua mbele kwenye mchezo huo, dakika ya 46.
Lakini Athumani Macheppe alizima shangwe za wana Yanga zikiwa zimesalia dakika mbili mchezo huo kumalizika kwa bao lake safi.
Sahau
kuhusu Akida, kama yupo mchezaji ambaye aliyewapa raha mashabiki wa
timu zote hizo, basi ni Said Nassor Yussuf Mwamba (pichani), maarufu
kama Kizota enzi zake, aliyefariki dunia Februari 11, mwaka 2007. Kizota
ni mchezaji aliyewasisimua kwa namna yake mashabiki wa Yanga na Simba
kutokana na mabao yake.
Kizota
alifariki dunia baada ya kugongwa na gari eneo la Veterinary, akiwa
anatoka kushuhudia mchezo wa marudiano, Kombe la Shirikisho la Soka
Afrika, Raundi ya Awali kati ya wenyeji Simba dhidi ya Textil de Pungue
ya Msumbiji. Alitoka kwa huzuni uwanjani siku hiyo baada ya kushuhudia
timu yake ya zamani, Simba ikitolewa na wageni kwa mikwaju ya penalti
3-1, kufuatia sare ya jumla ya 2-2.
Mchezo
wa kwanza Msumbiji, Simba ililazimisha sare ya 1-1 na marudiano nayo
pia walibanwa kwa sare aina hiyo hiyo, hivyo kufanya mshindi aamuliwe
kwa mikwaju ya penalti. Ntota ya timu ya kiwanda cha nguo Msumbiji ndiyo
iliyong’ara jioni hiyo.
Kama
kuna miaka ambayo Kizota alifanya vitu vya ‘babu kubwa’ kwenye soka ya
Tanzania, basi ni 1993, kwani mapema tu mwaka huo aliibuka mfungaji bora
kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati mjini Kampala,
Uganda, akiiwezesha Yanga pia kutwaa ubingwa wa michuano hiyo kwa
kuwafunga wenyeji, SC Villa.
Lakini
pia, alikuwa mfungaji bora wa Ligi ya Tanzania. Yote tisa, kumi ni pale
Kizota alipofunga mabao mawili peke yake, wakati Yanga inaibuka na
ushindi wa 2-1 dhidi ya Simba kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi ya
Tanzania Bara, Uwanja wa Taifa, (sasa Uhuru) mjini Dar es Salaam.
Ilikuwa
ni Machi 27, mwaka huo 1993, wakati Kizota alipomchambua kipa hodari
nchini enzi hizo, Mwameja Mohamed katika dakika za 47 na 57.
Simba
ikielekea kulala 2-0, shukrani kwake Edward Chumila (naye marehemu pia)
aliyewafungia Wekundu wa Msimbazi bao la kufutia machozi, dakika ya 75.
Baada
ya kipigo kikali cha mabao 4-1, Julai 2, mwaka 1994, Yanga ilivunja
kikosi ikiwafukuza karibu nyota wake wote wa kikosi cha kwanza kwa
tuhuma za kuhusika kuihujumu timu katika kipigo hicho kilichotokana na
mabao ya George Masatu, Athumani China, Madaraka Selemani na Dua Saidi,
bao la kufutia machozi la Yanga likifungwa na beki imara, Constantine
Kimanda.
Kati
ya nyota waliotupiwa virago Yanga ni Kizota, ambaye kutokana na makali
yake wakati huo, akiwa tegemeo la timu ya taifa ya Tanzania na miongoni
mwa nyota waliotoa mchango mkubwa kwenye kikosi kilichochukua Kombe la
Challenge nchini Kenya, Simba wakamwambia: “Usipate tabu Said, njoo
upumzike huku”.
Kizota
alitaka kuwaonyesha Yanga kwamba, walifanya kosa kumwacha na katika
mchezo wa marudiano baina ya watani hao wa jadi wa Ligi Kuu ya Bara,
Oktoba 4, 1995, Yanga ikiwa inaelekea kabisa kushinda mchezo huo 1-0,
Said Mwamba alitibua furaha ya wana Jangwani dakika ya 70 kwa kufunga
bao safi la kusawazisha.
Yanga
ilitangulia kupata bao kupitia kwa mpachika mabao wake mahiri enzi
hizo, Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ dakika ya 40. Bao la Kizota
liliwachanganya Yanga na dakika tisa baadaye, wakapachikwa bao la pili.
Safari hiyo alikuwa ni Mchunga Bakari ‘Mandela’ aliyewaambia wana
Jangwani; kutangulia si kufika.
Baada
ya msimu huo, Yanga walikiri kosa lao na wakaenda kumpigia magoti
Kizota arejee nyumbani. Kwa sababu Kizota alikuwa anaishi nyumba ya pili
kutoka klabu ya Yanga, akiishi na mkewe Tosha, Mtaa wa Jangwani, hivyo
ilikuwa rahisi kumrubuni na kurejea nyumbani.
Na
aliporejea Yanga, Kizota aliifunga tena Simba. Ilikuwa Novemba 9, mwaka
1996, katika sare ya ajabu ya watani, ya mabao 4-4 mjini Arusha.
Kizota
aliifungia Yanga bao la kusawazisha lililofanya sare ya 3-3 katika
dakika 70, baada ya awali Kipese kuifungia Simba, dakika ya saba,
Edibily Lunyamila kuisawazishia Yanga kwa penalti dakika ya 28, Ahmed
Mwinyimkuu kuifungia Simba la pili dakika ya 43, kabla ya Dua Said
kufunga la tatu dakika ya 60 na Mustafa Hoza kuisawazishia Yanga kwa
kujifunga dakika ya 64.
Sanifu
Lazaro aliifungia Yanga bao lililoelekea kuwa la ushindi dakika ya 75,
lakini walishindwa kulinda lango lao na kuruhusu bao la dakika za lala
salama, lililofungwa na Duwa Said dakika ya 90, hivyo kuwa sare ya 4-4.
Kizota
alijiunga na Yanga mwaka mwaka 1988, akitokea timu ya Shirika la Posta
la Tabora, enzi hizo likijulikana kama Posta na Simu, wakati akicheza
kama kiungo.
Baada
ya kung’ara akiwa na Yanga, msimu wa 1988 ulipomalizika alichukuliwa na
Al-Jazira ya Abu Dhabi, Falme za Kiarabu. Akiwa Abu Dhabi katika timu
yake mpya, Kizota alikutana na aliyekuwa nyota wa timu ya Taifa ya
Malawi, Lawrence Waya, ambaye alikuwa winga machachari sana enzi zake.
Kwa pamoja Kizota na Waya waliifanya timu yao kuwika mno katika soka ya
Uarabuni.
Kutokana
na vitu vyake vya uhakika, Kizota alikubalika mno na mashabiki wa soka
Abu Dhabi, jambo ambalo lilifanya Waarabu waanze kumrubuni abadili uraia
na kuwa raia wa huko. Ghiliba hizo hakupewa Kizota peke yake, bali hata
Waya.
Kizota
aliingiwa na ghiliba hizo na kuanza kufanyiwa taratibu za kupewa uraia,
lakini wakati taratibu zikifanywa, mwanasoka huyo aliomba likizo ya
kurejea nyumbani Tanzania kuoanana na familia yake na ndipo alipobadili
mawazo ya Uarabu. Hiyo ilikuwa ni mwaka 1989.
“Hakuna
kingine ni Yanga tu, nilipofika tu viongozi wakasema wananihitaji sana,
hivyo nikaamua kubaki Yanga,” aliniambia Kizota nilipozungumza naye
mwaka 1999. Kizota aliingia kwa makeke, safari hiyo hakuwa kiungo, bali
alihamia kwenye nafasi ya ushambuliaji na kufanikiwa kuipeleka Yanga
kileleni kwa mabao yake.
Hata
hivyo, viongozi wa timu yake baada ya kuona kimya kimezidi, walimtaka
haraka sana kurejea. Alitumiwa ujumbe wa simu ya maandishi (Fax) ambao
aliupuuza, lakini baadaye alifuatwa na viongozi hao walioondoka naye
kurejea Abu Dhabi.
Kizota
aliondoka nchini akiwa anaongoza kufunga mabao na Ligi imefikia
ukingoni, huku Yanga ikihitaji pointi chache tu kutangaza ubingwa, jambo
ambalo liliwezekana, licha ya yeye kuondoka na vijana wa Jangwani
kurejesha taji walilopokonywa na Coastal Union ya Tanga mwaka 1988.
Kizota
aliishi Uarabuni hadi mwaka 1991, aliporejea kupumzika na kuikuta Yanga
ikiwa katika hali mbaya, soka ya Tanzania inatawaliwa na watani wao wa
jadi, Simba, ambayo mwaka huo wakati anarejea (Simba) ilikuwa imetangaza
ufalme wa soka kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati, sasa Kombe la
Kagame.
“Kama
nilivyokwambia naipenda sana Yanga, nikaamua kubaki, lakini jamaa
(Al-Jazira) walikuwa wakinitaka nirejee haraka sana, nikawadanganya
naumwa, wakati wananitumia fedha za matibabu, kumbe mie niko safi
kabisa,” aliniambia Kizota, aliyehitumu elimu yake ya msingi mwaka 1981
katika shule ya Mabatini, Tabora alikozaliwa.
Kizota
aling’ara Yanga tangu mwaka huo, akiiwezesha kutwaa Kombe la Kagame
mwaka 1993, kufika fainali ya michuano hiyo mwaka 1992, Nusu Fainali
nchini Sudan mwaka 1994, kabla ya 1994 kuhamia Simba.
Aliporejea
Yanga 1996, alicheza kwa misimu miwili zaidi kabla ya mwaka 1998
kutimkia Al-Nasar ya Oman. Alikaa huko msimu mmoja tu, kabla ya kurejea
nchini katikati ya msimu wa Ligi Kuu na kujiunga na timu iliyokuwa
Daraja la Kwanza, Kariakoo United ya Lindi, ambako akiwa na wakongwe
wenzake kama Mustafa Hoza waliipandisha Ligi Kuu.
Baada
ya kuipandisha timu hiyo, Kizota alirejea Yanga ambako aliiwezesha timu
hiyo kutwaa Kombe la Kagame tena Uganda mwaka 1999, ingawa kutokana na
umri wakati huo, alirejea kucheza nafasi ya ulinzi. Hadi anafariki
dunia, Kizota alikuwa mume wa Tosha na baba wa watoto wawili, Hamim na
Rabii.
Source:Shafii